Tanzania: Upinzani walaani Lissu kuvuliwa ubunge lakini wasema bado uko imara

Tundu Lissu
Image caption Tundu Lissu

Siku moja baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, kulitangazia bunge la nchi hiyo kuwa ameiandikia tume ya uchaguzi kuileza kuwa jimbo la Singida Mashariki, lililokuwa likishikiliwa na mwanasiasa mwandamizi wa upinzani, Tundu Antipas Lissu Lissu kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema lipo wazi gumzo kuhusu hatua hiyo bado linaendelea.

Watu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kutoa maoni yao huku maswali kadhaa yakiibuliwa ikiwa ni pamoja na Spika Ndugai kumuonea Lissu, hana huruma na kwamba amekiuka sheria.

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe amesema uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai halijawatikisa wala kuwakatisha tamaa bali kuzidi kuimarisha dhamira yao ya kushika dola.

Akizungumza na gazeti la mwananchi, Bw. Mbowe alisema:"Wanatupa sababu zaidi za kufanya kazi vitu kama hivi haviwezi kutukatisha tamaa, vinatuimarisha katika dhamira yetu, tunafanyiwa uonevu mwingi

ndani ya bunge, tunafanyiwa visa vingi. Hivi visa havituvunji moyo,vinatuimarisha."

Image caption Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe (kulia)

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema, "Hasira ya kufukuza wabunge wetu, hasira ya kutoheshimu mawazo yetu, hasira ya kuondoa michango yetu tutaimaliza kwa kupeleka wabunge wengi, kuondoa wingi wa CCM ndani ya bunge na kuiongoza serikali ya nchi hii."

Baadhi ya wabunge wa upinzani nchini Tanzania pia wametoa maoni kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii kufuatia uamuziwaSpika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

kutangaza kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kilichokuwa kikikaliwa na Tundu Lisu wa Chadema kiko wazi.

Chama cha ACT wazalendo kimeandiika katika mtandao wake wa Twitter kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa ukandamizaji dhidi ya upinzani.

Waziri wa zamani wa maliasili na utalii nchini Tanzania, Lazaro Nyalandu pia ametoa kauli yake kuhusu hatua ya Bw. Lisu kuvuliwa ubunge akisema kuwa kitenndo hicho ''ni aibu kwa Tanzania''

Katika ukurasa wake wa akaunti ya Twitter aliandika "Kitendo cha Mh. Spika kumvua Ubunge Mh. @tundulisu huku akiwa anaendelea na matibabu Ubelgiji kufuatia shambulio dhidi yake la kupigwa risasi ni aibu na fedheha kwa demokrasia. Tundu Lissu ameonewa sana, haipendezi kuendelea kumuumiza zaidi. Hakika haki huinua Taifa. #BungeTZ."

Spika Ndugai alitangaza uamuzi huo jana Ijumaa Juni 28,2019 kabla ya kuahirisha mkutano wa 15 wa Bunge la Bajeti akisema Lissu amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na sababu mbili

za kutokutoa taarifa kwake (spika) na kutojaza fomu za mali na madeni kwa viongozi wa umma.

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa aliandika, "Hatua ya kuufuta ubunge wa Tundu Lissu, ni kuuonyesha ulimwengu jinsi ambavyo hatuna tena ubinadamu

na jambo hili halina tija kwa Serikali ya awamu ya tano wala kwa CCM yenyewe."

Haki miliki ya picha TWITTER @MSIGWAPETER
Image caption Mbunge wa Iringa Peter Msigwa

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema),John Heche ameandika katika ukurasa wake wa Twiter, "Katika maisha yangu sijawahi kushuhudia unyama wa kiwango hiki,"

"Lissu alipigwa risasi mchana kweupe wakati wa vikao vya bunge, hakuna mtu amekamatwa mpaka sasa, hakuna mtu alienda kumuona hospitali akiwemo spika mwenyewe....Leo

wanamvua ubunge?"aliuliza Heche.

Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Godbless Lema kwenye ukurasa wake wa Twiter aliandika kuwa "Mh Spika umemvua Mh Tundu Lissu Ubunge? Moyo wangu unavuja damu....Mungu

nisaidie,"

Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu Profesa J, aliandika katika akaunti yake ya Twitter, aliandika kando ya picha ya Lissu akisema: "Tabasamu tu kamanda Lissu, Mungu akiwa Upande wako wala Hakuna kitakachokushinda, hakika watashindana sana na neema za Mungu lakini kamwe hawatashinda.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Lissu amekuwa nje ya Tanzania kwa matibabu toka Septemba 2017, amsema tarejea nyumbani atakaporuhusiwa na madaktari wake.

Bw. Lissu ameiambia BBC kuwa ataenda mahakamani muda mfupi baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, kulitangazia bunge la nchi hiyo Ijumaa Juni 28 kuwa ameiandikia tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kuileleza kuwa jimbo la Singida Mashariki, lililokuwa likishikiliwa na Lissu kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema lipo wazi.

Mwanasiasa huyo pia ameiambia BBC kuwa yeye si mtoro bungeni na yungali anapokea matibabu barani Ulaya.

Spika Ndugai ametaja sababu kuu mbili zilizomsukuma kuiandikia tume ya uchaguzi barua hiyo, mosi ni kutokana na Lissu kutokuhudhuria bungeni kwa muda mrefu na pili kutokuwasilisha fomu ya tamko la mali na madeni kwa sekretari ya maadili kwa mujibu wa sheria.

Lakini Lissu amezipinga hoja zote mbili, akisema hashangazwi na tamko la Spika Ndugai.

"Mimi si mtoro bungeni na sijawahi kuwa mtoro. Kilichonikuta kinajulikana, nilipigwa risasi 16 nikiwa natoka bungeni Septemba 7, nikaletwa nje kwa matibabu. Tangu hapo nipo nje natibiwa," amesema Lissu na kuongeza, "Kwanza walionishambulia mpaka sasa hawajulikani, hakuna aliyekamatwa. Leo inasemwa sijulikani nilipo navuliwa ubunge... kinachoendelea si ajabu, kuna watu hawana maarifa tena, walichobaki nacho ni mabavu tu."

Huwezi kusikiliza tena
Tundu Lissu: Kushambuliwa kwangu kulichochewa na siasa Tanzania

Japo inafahamika kuwa mwanasiasa huyo alilazimika kusafirishwa nje ya Tanzania awali nchini Kenya na kisha Ubelgiji kwa matibabu baada ya shambulizi dhidi yake, kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya kutokuwepo kwake bungeni kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Hivi karibuni ikiwa yungali ughaibuni amezuru nchi za Marekani, Ujerumani na Uingereza, kote huko, amehojiwa na vyombo vya habari za kutoa mihadhara kwenye vyuo vikuu juu ya hali ya haki za binaadamu Tanzania.

Spika Ndugai mwezi Februari mwaka huu alikubali kufanyia kazi hoja ya kuzuia stahiki zake kama mshahara kwa madai hayo, na kusema kuwa hana taarifa rasmi juu ya alipo Lissu na hali yake ya kiafya, na amekuwa akimuona kwenye vyombo vya habari.

Lissu amesema nini hasa?

"Ni aibu kwa Spika wa Bunge kusema hajui nilipo, ilhali dunia nzima inajua nipo Ubelgiji na naendelea na matibabu. Kila siku mimi naenda hospitali kufanya tiba ya mazoezi, siwezi kutembea bila kufanya mazoezi hayo," amesema Lissu na kuongeza; "Ofisi ya bunge inajua fika niipo. Katibu wa Bunge ameshawahi kuwasiliana kwa barua na kaka yangu kuhusu matibabu yangu na nakala ya barua iliyotumwa na katibu ilinifikia nikiwa hospitali Ubelgiji. Wanajua nilipo."

Lissu amesema kufuatia kauli hiyo ya Spika, anawasiliana na mawakili wake nchini Tanzania ili wamwandikie kuomba nakala ya barua alotuma tume ya uchaguzi na pia kuiomba tume hiyo iwape nakala ya barua kutoka kwa Spika.

Hatua itakayofuata baada ya hapo ni kulifikisha suala hilo Mahakama Kuu.

"Tunaenda Mahakama Kuu ili iseme kama kweli Spika hajui nilipo, na kwa nini sipo Bungeni. Pia iseme kwa mazingira yangu na yaliyonikuta kama jimbo lipo wazi," amesema Lissu.

Lissu anaamini hatua ya Spika imekuja wakati huu kwa sababu ametangaza kuwa atarejea Tanzania mwezi wa tisa.

"Hawa watu wana hofu juu yangu, wana hofu juu ya Septemba 7 siku nitakayorudi Tanzania. Siku ambayo itatimu niaka miwili kamili toka niliposhambuliwa. Hakuna cha kunizuia kurudi," amesisitiza.

Lissu alikuwa miongoni mwa wanansiasa wa upinzani waliopendelea kumuita Magufuli kuwa 'Dikteta Uchwara' ama kwa lugha ya kingereza'Petty Dictator'.

Baada ya shambulio hilo, alikimbizwa Nairobi kwa matibabu kisha Brussels Ubelgiji toka mwezi Januari mwaka 2018.

Huko kote aliendelea kusisitiza kuwa serikali ya Magufuli ilikuwa na mkono kwenye shambulio dhidi yake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii