Tanzania yavunja mkataba na kocha Emmanuel Amunike

Amunike Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Amunike alipewa kibarua cha kuinoa Tanzania maarufu kama Taifa Stars mwezi Aprili 2018.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo Jumatatu Julai 8 limetangaza kusitisha mkataba na kocha Emmanuel Amunike.

Taarifa fupi iliyotolewa na TFF inadai kuwa Amunike amekubaliana na TFF kusitisha mkataba huo.

Shirikisho hilo pia limesema pia litatangaza Kocha wa muda atakaekiongoza Kikosi cha Timu ya Taifa kwa mechi za CHAN.

"Makocha wa muda watatangazwa baada ya Kamati ya Dharura ya Kamati ya Utendaji (Emergency Committee) itakapokutana Julai 11,2019," inasema taarifa ya TFF.

Mchakato wa kutafuta Kocha mpya umeanza mara moja.

Amunike alipewa kibarua cha kuinoa Tanzania maarufu kama Taifa Stars mwezi Aprili 2018.

Atabakia kwenye historia ya mpira Tanzania kwa kuingoza nchi hiyo kufuzu kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya miaka 39.

Kabla ya hapo alinyanyua Kombe la Dunia 2015 akiwa kocha wa timu ya vijana wa chini ya miaka 17 Nigeria.

Haki miliki ya picha Getty Images

Kocha huyo ni winga wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria na klabu ya Barcelona.

Hata hivyo, Amunike amekuwa akilaumiwa na baadhi ya mashabiki kwa namna anavyoteua wachezaji na kupanga kikosi.

Katika mashindano yanayoendelea nchini Misri, Tanzania ilitolewa baada ya kupoteza michezo yote ya makundi.

Tanzania ndiyo timu iliyofanya vibaya zaidi katika mashindano hayo kitakwimu kwenye hatua ya makundi.

Tanzania imefungwa jumla ya magoli nane na kufunga mawili, hivyo wamemaliza wakiwa na uwiano wa magoli -6.

Timu inayofuata kwa kufanya vibaya ni Namibia ambayo pia ilifungwa mechi zote na kumaliza na uwiano wa magoli -5, kisha Burundi yenye alama sifuri pia na uwiano wa magoli -4.

Usia wa Amunike kwa Tanzania

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Amunike alipewa kibarua cha kuinoa Tanzania maarufu kama Taifa Stars mwezi Aprili 2018.

Kabla ya mkataba wake kuvunjwa, Amunike alisema kutolewa mapema nchini Misri ilikuwa ni funzo kubwa kwa Tanzania.

"Ni somo kubwa kwa mpira wa Tanzania. Hatukuwahi kushiriki toka mwaka 1980, mambo mengi yametokea ndani ya miaka 39, na mpira umebadilika na unaendelea kubadilika," Amunike aliiambia BBC.

"Kitu cha msingi ni kuendana na mabadiliko haya na kuimarika kama timu. Kuna mengi ya kujifunza.

"Shida yetu kubwa ilikuwa ni kutokuwa na uzoefu. Hatuna uzoefu wa kutosha sababu tumezoea kucheza mpira bila kuwa na shinikizo kubwa."

"Lakini tumeona katika michuano hii pale unapokuwa na mpira, basi wapinzania wanakuweka katika shinikizo kubwa."

"Katika kila safari, kuna mchakato wa kujifunza. Tutakaporejea (nyumbani) itatupasa tujitathmini kwa undani na kuona ni kwa namna gani tutaboresha mpira wetu.

"Ni dhahiri kuwa katika mpira wa kisasa, kama huna uwezo wa kushindana hutakuwa na nafasi ya kushinda - na hilo ndilo tulilokutana nalo."

"Kama tutaendelea na ari hii, na kuboresha katika yale tufanyayo naamini tutakuwa kama timu."