Neymar Jr: Mshambuliaji huyo wa Brazil asusia mazoezi - klabu kumchukulia hatua kali

Neymar Jr Haki miliki ya picha AFP

Paris St-Germain imesema kuwa itachukua hatua kali baada ya mshambuliaji wa Brazil Neymar kufeli kuhudhuria mazoezi ya kwanza ya timu hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alitarajiwa kurudi katika mazoezi siku ya Jumatatu.

Mshambuliaji huyo amehusishwa na uhamisho kurudi klabu yake ya zamani ya Barcelona.

"Paris St-Germain imesema kuwa Neymar Jr hakuhudhuria kikao cha kwanza cha mazoezi kulingana na muda na eneo la mazoezi hayo.

''Hii ni kinyume na matarajio ya klabu hiyo'' , ilisema taarifa.

''Klabu hii inajutia hatua hiyo''.

Je Naymar ana mpango gani?

Neymar alijiunga na PSG kutoka Barcelona kwa dau lililovunja rekodi la £200m mnamo mwezi Agosti 2017.

Ameifungia klabu hiyo magoli 34 katika mechi 37 na kuisaidia kushinda mataji ya ligi ya kwanza lakini pia amehusishwa na makosa kadhaa ya utovu wa nidhamu ikiwemo kupigwa marufuku kwa mechi tatu kwa kumkemea shabiki baada ya PSG kushindwa katika kombe la ligi ya Ufaransa.

Pia atakosa kushiriki mechi tatu za Ulaya kwa kumtusi afisa wa mechi.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Santos nchini Brazil alivuliwa unahodha mnamo mwezi Mei kabla ya kupata jeraha la kifundo cha mguu wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Qatar ambayo ilimfanya kukosa michuano ya Copa America ambayo taifa lake ndilo lililoibuka mshindi nyumbani.

Wiki iliopita rais wa Barcelona Josep Bartomeu alidai kwamba Neymar anataka kuondoka PSG msimu huu.

Kulingana na ripoti katika vyombo vya habari vya Uhispania , Neymar amekubali kupunguziwa mshahara wake kwa Yuro 12m ili kusaidia katika kurudi katika klabu yake ya zamani katika uwanja wa Nou Camp ambapo alicheza kati ya mwaka 2013 hadi 2017.

Mabingwa hao wa Catalan tayari wamewasajili Frenkie de Jong kutoka Ajax kwa dau la £67m msimu huu na wanadaiwa kuwa na hamu ya kumsaini mshambuliaji wa Ufaransa Antoine Griezmann kutoka Atletico Madrid.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii