PSG: Neymar anaweza kuondoka akipata ofa itakayomfurahisha

Ameifungia klabu hiyo magoli 34 katika mechi 37 na kuisaidia kushinda mataji ya ligi ya kwanza lakini pia amehusishwa na makosa kadhaa ya utovu wa nidhamu

Neymar anaweza kuondoka PSG iwapo kutakuwa na ofa itakayomfurahisha , amesema mkurugenzi wa michezo katika klabu hiyo Leonardo.

Mshambuliaji huyo wa Brazil alisusia mazoezi ya kwanza ya klabu hiyo msimu huu siku ya Jumatatu na PSG imesema kuwa itamchukulia hatua kali za kinidhamu.

Mchezaji huyo amehusishwa na uhamisho wa kurudi katika klabu yake ya zamani Barcelona.

Leonardo aliongezea kwamba mabingwa hao wa Ufaransa walikuwa hawajapokea ofa zozote za Neymar lakini kumekuwa na 'mawasiliano' yasio rasmi kutoka kwa Barcelona.

Je Naymar ana mpango gani?

Neymar alijiunga na PSG kutoka Barcelona kwa dau lililovunja rekodi la £200m mnamo mwezi Agosti 2017.

Alipoulizwa iwapo mchezaji huyo alitaka kuondoka , Leonardo akizungumza na gazeti la Parisien alisema: Ni wazi kwa kila mtu.

''Lakini katika soka unasema kitu kimoja leo kesho unasema chengine. Ndio nimezungumza na Neymar. Sitaki kuytoa maelezo yote ya mazungunzo yetu. Pia tulizungumza na maajenti wake. Kila mtu anajua kila kitu. Msimamo ni wazi kwa kila mtu.lakini kitu kimoja kiko wazi bado ana kandarasi ya miaka mitatu nasi.Na kwa sababu hatujapokea ofa yoyote hatuwezi kujadiliana chochote''.

Aliongezea: Neymar anaweza kuondoka PSG iwapo kuna ofa inayomurahisha. Lakini kufikia leo, hatujaona mtu yeyote ambaye ametaka kumnunua na hata dau linalotolewa. Mambo yote haya hayafanyiki kwa siku , huo ndio ukweli. PSG inataka kuwategemea wachezaji ambao wanataka kusalia na kutengeza kitu kikubwa. Hatutaki wachezaji ambao wangefurahisha klabu iwapo wangesalia.

Je Neymar yuko wapi?

Vyombo vya habari vya Brazil vilimnukuu babake Neymar akisema kuwa PSG ilifahamu kwamba mchezaji huyo asingehudhuria mazoezi siku ya Jumatatu kutokana na majukumu mengine ya wakfu.

''Sababu ilijulikana na kupangwa kwa mwaka ikiwa ni miongoni ya mambo anayofanyia wakfu wake wa Neymar Institute '', Neymar Snr aliambia Fox Sports Brazil.

''Hatukuweza kuahirisha na atarudi PSG tarehe 15 Julai'.

Hatahivyo Leonardo alisema kuwa hakuna tarehe zilizokubaliwa na klabu hiyo.

"Paris St-Germain imesema kuwa Neymar Jr hakuhudhuria kikao cha kwanza cha mazoezi kulingana na muda na eneo la mazoezi hayo.

''Hii ni kinyume na matarajio ya klabu hiyo'' , ilisema taarifa.

''Klabu hii inajutia hatua hiyo''.

Ameifungia klabu hiyo magoli 34 katika mechi 37 na kuisaidia kushinda mataji ya ligi ya kwanza lakini pia amehusishwa na makosa kadhaa ya utovu wa nidhamu ikiwemo kupigwa marufuku kwa mechi tatu kwa kumkemea shabiki baada ya PSG kushindwa katika kombe la ligi ya Ufaransa.

Pia atakosa kushiriki mechi tatu za Ulaya kwa kumtusi afisa wa mechi.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Santos nchini Brazil alivuliwa unahodha mnamo mwezi Mei kabla ya kupata jeraha la kifundo cha mguu wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Qatar ambayo ilimfanya kukosa michuano ya Copa America ambayo taifa lake ndilo lililoibuka mshindi nyumbani.

Wiki iliopita rais wa Barcelona Josep Bartomeu alidai kwamba Neymar anataka kuondoka PSG msimu huu.

Kulingana na ripoti katika vyombo vya habari vya Uhispania , Neymar amekubali kupunguziwa mshahara wake kwa Yuro 12m ili kusaidia katika kurudi katika klabu yake ya zamani katika uwanja wa Nou Camp ambapo alicheza kati ya mwaka 2013 hadi 2017.

Mabingwa hao wa Catalan tayari wamewasajili Frenkie de Jong kutoka Ajax kwa dau la £67m msimu huu na wanadaiwa kuwa na hamu ya kumsaini mshambuliaji wa Ufaransa Antoine Griezmann kutoka Atletico Madrid.