Julian Draxler: Ubinafsi wa wachezaji wa PSG ni mzigo kwa timu

Paris St-Germain forwards Neymar (left), Edinson Cavani (centre) and Kylian Mbappe Haki miliki ya picha Getty Images

"Ubinafsi" wa baadhi ya wachezaji nyota wa klabu bingwa nchini Ufaransa Paris St-Germain "unafanya mambo yawe magumu kwa timu yote", amesema winga wa klabu hiyo Julian Draxler.

Draxler ambaye ni raia wa Ujerumani anacheza kwenye klabu hiyo pamoja na nyota kadhaa wakiwemo Neymar - ambaye amekuwa akihusishwa na harakati za kurudi Barcelona - Kylian Mbappe na Edinson Cavani.

"Wachezaji wote hao ni wa kiwango kikubwa, ni vigumu kupata wachezaji wa kiwango hiki," Draxler ameiambia AFP.

"Lakini wote wana vichwa vyao na akili zao. Wanauishi mpira, wanataka kufunga kwenye kila mechi, hivyo wanaubinafsi.

"Wakati mwengine (ubinafsi huo) hufanya mambo yawe magumu kwa timu nzima, lakini ukipata bahati ya kucheza nao, itakuwa ni jambo kubwa kwako kila siku."

Haki miliki ya picha Getty Images

Mkurugenzi wa michezo wa PSG Leonardo amesema Neymar anaweza kuondoka klabuni hapo "endapo itapatikana ofa itakayomridhisha kila mtu" baada ya mchezaji huyo kushindwa kuhudhuria siku ya kwanza ya mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao hivi karibuni.

Neymar alijiunga na PSG kutoka Barcelona kwa dau lililovunja rekodi la £200m mnamo mwezi Agosti 2017, lakini inaarifiwa kuwa hana furaha tena klabuni hapo.

Hatahivyo, mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Brazil yupo kwenye kambi ya timu hiyo inayofanya ziara nchini Uchina.

Mada zinazohusiana