Romelu Lukaku: Inter Milan waafikiana bei na Man United

Romelu Lukaku Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Romelu Lukaku amefunga magoli 42 katika mechi 96 alizoichezea Man United

Inter Milan na Manchester United wameafikiana kuhusu usajili wa mshambuliaji Romelu Lukaku.

Inter sasa itatoo kitita cha pauni milioni 74, dau ambalo Man United walikuwa wakilitaka toka awali.

Mwezi Julai, United ilikataa dau la pauni milioni 54 kwa ajili ya usajili wa Lukaku kwenda Inter.

Lukaku amepigwa faini na United baada ya kukicha mazoezi ya timu hiyo bila ruhusa ya uongozi, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake kuchochea uhamisho.

Mchezaji huyo amekuwa akifanya mazoezi na klabu yake ya zamani Anderlecht kwa siku mbili zilizopita.

Ajenti wa Lukaku, Federico Pastorello, alilazimika kwenda jijini London jana ili kukutana na wawakilishi wa Man United ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Usiku wa jana, Pastorello alituma picha katika mtandao wake wa Instagram akiwa kwenye ndege na Lukaku na kuandika maelezo yafuatayo: "Tayari kwa kupaa. Muelekeo Milano."

Inter na United wamekuwa wakivutana kwa wiki kadhaa juu ya thamani halisi ya mchezaji huyo, huku United ikitaka walau kurejesha pauni milioni 75 ambazo walitumia kumsajili miaka miwili iliyopita, na sasa wamefanikiwa.

Kocha wa Inter, Antonio Conte alitangaza toka awali kuwa Lukaku ndiye kipaumbele chake cha kwanza kwenye dirisha hili la usajili. "Ninamchukulia kama mchezaji ambaye anaweza kuboresha kikosi chetu," amesema Conte.

Lukaku alihamia United 2017 akitokea Everton huku kukiwa na shauku kubwa juu ya kipaji chake na mchango wake kwenye timu hiyo.

Wakati huo, alikuwa ni mchezaji wa nne wa chini ya miaka 24 kufunga magoli zaidi ya 80 katika ligi ya Primia. Wengine ni Wayne Rooney, Robbie Fowler na Michael Owen.

Katika msimu wake wa kwanza Old Trafford, Lukaku alifunga magoli 27, hata washambuliaji hatari wa zamani wa klabu hiyo kama kocha wa sasa Ole Gunnar Solskjaer, Cantona na Andy Cole hawakupata mafanikia ya namna hiyo kwenye msimu wa kwanza, maana wote walifunga magoli 25.

Hata hivyo asilimia 26 ya magoli yote ya Lukaku Man United aliyafunga kwenye miezi yake miwili ya kwanza.

Kwa ujumla, amefunga magoli 42 katika mechi 96 alizoichezea Man United.

Lukaku hakupewa nafasi ya kutosha na Solskjaer katika nusu ya pili ya msimu uliopita huku Marcus Rashford akitumika zaidi.

Mada zinazohusiana