Je, uhasama wa Mancester City na Liverpool kuendelea msimu huu?

Manchester City Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Manchester City watatetea ubingwa wao msimu ujao?

Pazia la Ligi Kuu ya England, maarufu kama Ligi ya Primia msimu wa 2019/2020 linafunguliwa rasmi hii leo.

Msimu uliopita 2018/2019 ulikuwa ni moja ya misimu bora na wenye ushindani wa hali ya juu, mambo yatakuwaje kwenye msimu mpya.

Mshindi wa Primia msimu uliopita Manchester City na mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Liverpool, walimaliza kwa kupishana kwa pointi moja tu katika ligi.

Liverpool ilimaliza msimu ikiwa na pointi 97, ambazo ni nyingi kuwahi kukusanywa na mshindi wa pili. Jurgen Klopp atataka kuhakikisha anampiku Pep Guardiola safari hii.

Msimu wa 2019/19 Liverpool na Manchester City walibadilishana nafasi ya kileleni zaidi ya mara kumi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa EPL na kuonesha uhasama wa aina yake huku wakicheza kandanda ya kuvutia na kasi ya kusisimua.

Uhasama huo bila shaka utaendelea tena msimu huu na ushahidi ni mchezo wa 'kirafiki' wa Ngao ya Jamii ambao ulichezwa kama fainali kwenye uwanja wa Wembley, kila upande ukitaka kushinda mechi hiyo. Kwa Liverpool na City, unaweza kusema huu si msimu mpya kwao bali ni muendelezo wa msimu uliopita.

Liverpool walipoteza mchezo huo kwa matuta, baada ya kukosa mkwaju mmoja wa penati, lakini tulipata nafasi ya kuona kionjo cha jinsi msimu utakavyokwenda kwa timu hizi mbili ambazo ni kama 'wababe wapya' katika Ligi Kuu ya England ambayo ilikuwa ikitawaliwa na Manchester United, Chelsea na Arsenal katika robo karne iliyopita.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Safu ya ushambuliaji ya Liverpool ikiongozwa na Salah, Mane na Firminho inatarajiwa kuendeleza makali msimu huu.

Lakini sasa mtaani kuna 'vichwa' vipya, na katika takriban miaka kumi iliyopita, tunashuhudia kilele cha EPL kikianza kutawaliwa na waliyokuwa 'wanyonge'. Manchester City, Liverpool na Tottenham wameingia kwenye picha na hakuna dalili zozote zinazoonesha kuwa wataondoka hivi karibuni.

EPL ambayo kwa miaka mingi ikifahamika kuwa na 'Top 4" sasa imebadilika na kufika 'Top 6" kwa sababu ya ushindani ambao umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, hasa kutokana na kuingia kwa wababe wapya.

Nafasi tatu za juu, kama msimu uliopita, wengi wanatarajia kugombewa na Tottenham, Man City na Liverpool. Nafasi tatu zilizosalia za top 6 zinatazamiwa kugombewa na Arsenal, Chelsea na Manchester United.

Lakini kama tulivyoshuhudia msimu uliopita, nafasi hizo 'hazijathibitishwa' kwa sababu kuna timu kama Everton na Wolverhampton ambazo kwa jinsi zilivyocheza zinaweza kutikisa na kuingia ndani sita bora.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Je, Solskjaer ataweza kuingoza Man United mpaka kuchukua ubingwa msimu huu? Ama mashabiki wataendelea kusubiri?

Licha ya kuwa msimu huu fedha nyingi hazijatumika kwenye usajili ukilinganisha na misimu miwili iliyopita, utakuwa msimu mgumu hasa kwa mameneja wapya katika timu za juu- kama vile Frank Lampard, Ole Gunnar Solskjaer na hata Unai Emery ambaye unaweza kusema ndio kwanza anaunda kikosi chake baada ya miaka ishirini na ushee ya Profesa Arsene Wenger.

Kwa upande chini wa msimamo, katika miaka kumi iliyopita, timu mbili kati ya tatu zinazopanda daraja hufanikiwa kusalia kwenye ligi. Ni mara tatu tu katika historia ya Ligi Kuu ya England ambapo timu zote tatu zilizopanda daraja zilifanikiwa kuepuka kushuka daraja katika msimu ambao zilipanda.

Msimu huu VAR itatumika kwa mara ya kwanza na hivyo kuongeza chachu katika ligi hii maarufu na yenye ushindani duniani. Na sheria nyingine kadhaa pia zitatumika, ikiwemo ya kudhibidi mameneja 'wakorofi' kwa kuonesha kadi za manjano kama onyo na pia sheria na 'sub' ambapo wachezaji wanaobadilishwa hutakiwa kutoka uwanjani haraka kuepuka kupoteza muda.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Katika msimu huu, teknolojia ya usaidizi wa mwamuzi maarufu kama VAR itaanza kutumika England

Msimu ni mpya, na EPL miaka yote hushangaza wengi kwa kuleta kitu kipya, lakini kwenye karatasi unaweza kubashiri nani ana nafasi kubwa ya kuwa bingwa, na nani ana nafasi kubwa ya kushuka daraja. Hata hivyo burudani itakuwa katika timu zile ambazo zinataka kwa udi na uvumba kurejesha 'heshima' zake.

*BBC Ulimwengu wa Soka itakuwa ikikutangazia mechi za EPL kila Jumamosi na Jumapili kupitia redio washirika.

Mada zinazohusiana