Gareth Bale: Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane 'kumtegemea' mshambuliaji wa Wales

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane hana budi kumtegemea Bale
Image caption Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane hana budi kumtegemea Bale

Mkufunzi wa klabu ya ya Real Madrid Zinedine Zidane amesema sasa "anamtegemea" mshambuliaji Gareth Bale licha ya kauli alizozitoa awali kwamba nyota huyo wa kimataifa wa Wales huenda akahama klabu hiyo.

Bale alitarajiwa kujiunga na klabu ya Jiangsu Suning inayoshiriki Super League ya Uchina mwezi Julai.

Zidane wakati huo alisema kuondoka kwake kutakuwa vyema kwa kila mtu.

Mchezaji Eden Hazard aliyesajiliwa hivi karibuni aliumia paja siku ya Ijumaa akiwa mazoezini sasa Bale huenda akategemewa katika mechi ya ufunguzi wa La Liga dhidi ya Celta Vigo Jumamosi ya leo.

"Ilionekana kama ataondoka lakini kwa kuwa hakufanya hivyo nitamtegemea sawa na wachezaji wengine katika kikosi," alisema Zidane.

"Ana mkataba, na ni mchezaji muhimu, na kila mchezaji ananipatia wakati mgumu kuamua nani ajumuishwe katika kikosi cha kwanza au la."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gareth Bale (kulia)

Hazard, anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kati ya wiki tatu mpaka nne, huku Real ikiendelea kumudu bila uwepo wa muda mrefu wa Marco Asensio na beki wa kushoto Ferland Mendy ambaye anauguza jeraha.

Majeruhi hayo yanamaanisha mchezaji nyota wa Colombia James Rodriguez pia ana nafasi ya kuiwakilisha klabu hiyo katika mashindano ya msimu huu baada ya kuwa na Bayern Munich kwa mkopo wa miaka miwili.

"Yuko sawa, na ni vyema amerudi," aliongeza Zidane.

Bale mwenye miaka 30 alijiunga na miamba hiyo ya Uhispania kwa dau lililovunja rekodi la £85m kutoka Tottenham 2013. Amesalia na kandarasi ya miaka mitatu katika uwanja wa Bernabeu ambapo ameshinda mataji manne ya ligi ya mabingwa Ulaya , taji moja la la Liga, mataji matatu ya Uefa na mataji matatu ya klabu bora duniani.

Alifunga magoli matatu , pamoja na penalti katika fainali nne za ligi ya mabingwa baada ya kushinda kombe hilo 2014, 2016, 2017 na 2018.

Hata hivyo majeraha yamemkwaza katika misimu yote minne akiichezea Real Madrid.

Haki miliki ya picha Reuters

Aliichezea Real mechi 42 msimu uliopita lakini alizomelewa na mashabiki wa nyumbani katika mechi kadhaa .

Kurudi kwa Zidane katika timu hiyo kulidaiwa kuwa habari mbaya na ajenti wa mshambuliaji huyo Jonathan Barnett, kwa kuwa raia huyo wa Ufaransa hakutaka kufanya kazi na Bale na wawili hao walitofautiana kuhusu mfumo wa kucheza.

Bale alimaliza msimu uliopita kama mchezaji wa ziada wakati Real Madrid ilipoandikisha matokeo mabaya zaidi katika kipindi cha miaka 20 wakishindwa mara 12 na kupata pointi 68 na kuwa katika nafasi ya tatu - pointi 19 nyuma ya mabingwa Barcelona.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii