Mbwana Samatta: KRC Genk kuminyana na Napoli usiku wa leo

Samatta Haki miliki ya picha TF-Images
Image caption Samatta tayari ameshafunga goli moja kwenye michuano ya Champions League

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta usiku wa leo akiwa na klabu yake ya KRC Genk anatarajiwa kushuka dimbani kwa mchezo wake wa pili wa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (Champions League) dhidi ya Napoli.

Genk, itakuwa nyumbani Ubelgiji katika dimba la Luminus Arena ikiwakaribisha miamba kutoka Italia klabu ya Napoli.

Katika mchezo wake wa kwanza Genk iliangushiwa kichapo kizito cha goli 6-2 ugenini dhidi ya RB Salzburg, huku Samatta akifunga goli moja la kufutia machozi.

Katika mchezo huo, Samatta aliweka rekodi binafsi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Champions League na kufunga goli.

Napoli wao walianza kwa kuwafunga mabingwa watetezi Liverpool goli 2-0.

Hivyo, Genk hii leo watakuwa tena na kibarua kizito cha kuwazuia Napoli.

Hata hivyo, japo Genk haijawahi kupata ushindi hata mechi moja ya Champions League katika mara zote tatu walizoshiri michuano hiyo, wamefungwa mechi moja tu nyumbani kati ya sita walizocheza na kutoka sare tano.

Napoli pia hawajapata ushindi wakiwa ugenini kwenye hatua ya makundi ya Champions League katika mechi sita zilizopita. Hivyo, japo si ya kutumainia, historia inaweza kuwabeba Genk na kupata walau sare.

Image caption Kalidou Koulibaly alimkaba Samatta vilivyo Senegal ilipoifunga Tanzania 2-0 kwenye micuano ya Afcon.

Mechi ya leo pia itawakutanisha tena Samatta na beki kisiki Kalidou Koulibaly raia wa Senegal.

Wawili hao waliminyana kwenye michuano ya Afcon Juni 23mwaka huu ambapo Senegal ilipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania.

Je, Samatta ataweza kumpita Koulibally leo na kufunga goli baada ya kushindwa kufurukuta mbele yake Afcon?

Mechi hiyo itapigwa kuanzia saa mbili kasoro dakika tano za usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Tottenham yapigwa 7, Real Madrid yaponea chupuchupu

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Serge Gnabry alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Tottenham.

Katika michezo ya Champions League iliyopigwa jana usiku, klabu ya Tottenham ilipokea kipigo kizito cha 7-2 wakiwa nyumbani jijini London dhidi ya miamba ya Ujerumani Bayern Munich.

Kipigo hicho ni anguko kubwa kwa Tottenham ambao msimu uliopita walifika fainali ya michuano hiyo na kufungwa 2-0 na Liverpool.

Tottenham ndio walianza kupata bao katika mechi hiyo kupitia mshambuliaji Son Heung-Min ktika dakika ya 12, lakini Joshua Kimmich alisawazisha baada ya dakika tatu tu, Robert Lewandowski akaitanguliza Bayern katika dakika ya 45 na kipindi cha kwanza kuisha kwa matokeo ya 2-1.

Kipindi cha pili kilikuwa kichungu mno kwa Tottenham, na mshambuliaji Serge Gnabry alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya wenyeji.

Gnabry amecheka na nyavu za Spurs mara nne, na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga idadi hiyo ya magoli katika kipindi cha pili kwenye michuano ya Champions League.

Magoli yake alipachika katika dakika za53,55,83, 88.

Bao la pili la Tottenham lilipachikwa kwa mkwaju wa penati na nahodha Harry Kane. Lewandowsi alipachika bao lake la pili na la sita kwa Bayern katika dakika ya 87.

Katika dimba la Santiago Bernabeu, Real Madrid waliponea chupuchupu kufungwa mechi ya pili mfululizo na kufanikiwa kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Club Bruges ya Ubelgiji.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mshambuliaji kinda wa Nigeria Emmanuel Dennis ameichachafya safu ya ulinzi ya Madrid.

Mshambuliaji wa Nigeria Emmanuel Dennis aliitanguliza Club Brugges kwa magoli mawili ya kipindi cha kwanza (dakika ya 9 na 39).

Kipindi cha pili Real Madrid wakapata bao la kwanza katika dakika ya 55 kupitia Sergio Ramos, na dakika tano kabla ya mchezo kuisha, Casemiro akaisawazishia timu yake na kufanya matokeo kuwa 2-2 mpaka mwisho wa mchezo.

Kwa matokeo hayo, Madrid wanasalia mkiani mwa kundi A wakiwa na alama 1, hali inayoendelea kuuweka mustakabali wa kocha wao Zinedine Zidane katika wakati mgumu.

Mada zinazohusiana