Lionel Messi aibuka kuwa mshindi wa Ballon d'Or 2019

Messi ndio mshindi wa Ballon d'Or kwa mwaka 2019 Haki miliki ya picha EPA
Image caption Messi ndio mshindi wa Ballon d'Or kwa mwaka 2019

Mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka 2019 si mwingine bali ni Lionel Messi, ambaye amejichukulia kinyang'anyiro cha kuwa mchezaji bora zaidi kwa mara ya sita.

Mchezaji huyo wa Argentina mwenye miaka 32 amenyakua tuzo hiyo baada ya kuikosa toka mwaka 2015 na hii ni kutokana na kuweza kufunga mara 54 katika klabu ya nchini kwake kwa mwaka 2018-19 .

Virgil van Dijk alikuwa mshindi wa pili - yeye ni miongoni mwa wachezaji wanne wa Liverpool katika saba bora, akiwemo Sadio Mane.

Mchezaji wa Juventus Cristiano Ronaldo, aliwahi kutunukiwa tuzo hiyo mara tano na amekuwa watatu katika kura.

Toka mwaka 2008 tuzo hiyo maarufu zaidi ya wasakata kandanda duniani imetawaliwa na washambuliaji hatari katika kizazi cha sasa Messi na Ronaldo.

Mpaka kufikia mwaka 2017, kila mmoja wao akishinda mara tano.

Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa la Croatia Luka Modric aliingilia ufalme wa Messi na Ronaldo baada ya kunyakua tuzo hiyo mwaka jana.

Na sasa Messi amerejea kileleni kwa kumpiku Ronaldo na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kunyakua tuzo hiyo mara sita.

Image caption Hii ni mara ya tatu kwa Messi, Ronaldo na Van Dijk kuwania tuzo kwa pamoja mwaka huu.

Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa mwaka huu kwa Messi, Ronaldo na Van Dijk kuwania tuzo moja kwa pamoja.

Mara ya kwanza walikutana katika tuzo za Mchezaji Bora wa Ulaya (Uefa) mwezi Agosti ambapo Van Dijk aliibuka na ushindi.

Mara ya pili wakaminyana katika tuzo za Mchezaji Bora wa Fifa ambapo Messi aliibuka mshindi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mwaka jana, kiungo wa Real Madrid Luka Modric alikuwa mchezaji wa kwanza tofauti na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kushinda tuzo hiyo baada ya miaka 10.

Tano Bora ya Ballon d'Or

1. Leonel Messi (Barcelona na Argentina)

2. Virgil van Dijk (Liverpool na Uholanzi)

3. Cristiano Ronaldo (Juventus na Ureno)

4. Sadio Mane (Liverpool na Senegali)

5. Mohammed Salah (Liverpool na Misri)

Ballon d'Or ni nini?

Tuzo ya Ballon d'Or imekuwa ikitolewa nchini Ufaransa kila mwaka toka 1956, na mshindi wake wa kwanza alikuwa mchezaji kutoka Uingereza Stanley Matthews.

Awali tuzo hiyo ilikuwa ni kwa wachezaji wa Ulaya tu kabla ya kufanyika mabadiliko mwaka 1995 na kujumuisha wachezaji wa mataifa yote duniani, mradi wanasakata kandanda katika vilabu vya Ulaya.

Orodha ya majina ya wachezaji 30 bora huandaliwa na baadae kupigiwa kura na wanahabari wa michezo kutoka sehemu tofauti duniani, ambapo kila nchi hupiga kura moja.

Kutoka mwaka 2010 mpaka 2015 tuzo hiyo iliunganishwa na ile ya Fifa lakini zilitengana mwaka 2016 ambapo Fifa ilianza kundaa tuzo zao wenyewe.

Washindi wa Ballon d'Or : Ronaldo & Messi watawala kuanzia 2008
2008 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Fernando Torres
2009 Lionel Messi Cristiano Ronaldo Xavi
2010 Lionel Messi Andres Iniesta Xavi
2011 Lionel Messi Cristiano Ronaldo Xavi
2012 Lionel Messi Cristiano Ronaldo Andres Iniesta
2013 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Frank Ribery
2014 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Manuel Neuer
2015 Lionel Messi Cristiano Ronaldo Neymar
2016 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Antoine Griezmann
2017 Cristiano Ronaldo Lionel Messi Neymar
2018 Luka Modric Cristiano Ronaldo Antoine Griezmann
2019 Lionel Messi Virgil van Dijk Cristiano Ronaldo

Mada zinazohusiana