Carlo Ancelotti: Everton kucheza klabu bingwa si jambo linaloshindikana

Carlo Ancelotti

Chanzo cha picha, Getty Images

Kuigeuza Everton kuwa klabu ya kugombea nafasi ya kucheza Champions League si jambo ambalo halitawezekana, anaeleza kocha mpya wa klabu hiyo Carlo Ancelotti.

Ancelotti, 60, ambaye ni kocha wa zamani wa Chelsea, Real Madrid na AC Milan ametia saini mkataba wa kuwanoa Everton mpaka mwaka 2024.

Kocha huyo mwenye mafanikio lukuki anaichukua timu hiyo ikiwa nafasi ya 15 kwenye jedwali la Ligi ya Primia, wakiwa na alama nne tu juu ya mstari wa kushuka daraja.

"Champions League ni mpango wetu wa muda mrefu," amesema na kuongeza. "Hakuna kisichowezekana katika mpira wa miguu."

Everton hawajamaliza katika nafasi nne za juu toka mwaka 2005, na kabla ya hapo ilikuwa mwaka 1988.

Klabu pekee ambazo Ancelotti amefundisha na kukosa uwiano wa ushindi wa kufikia 50% ni klabu za Italia za Reggiana na Parma mwishoni mwa miaka ya 1990.

Ancelotti amesema kilichomvutia kujiunga na klabu hiyo ni: "Historia na utamaduni wa klabu. Ni moja ya klabu kubwa zaidi England."

Ancelotti ameshinda Champions League mara tatu kama kocha - mara mbili akiwa na AC Milan na mara moja na Real Madrid.

Pia ametwaa ubingwa wa Ligi ya Primia na Kombe la FA akiwa na Chelsea mwaka 2010 na ametwaa mataji wakiwa na Bayern Munich na Paris St-Germain.

Ancelotti ametua Everton siku chache baada ya kutimuliwa katika klabu ya Napoli ya nchini kwao Italia.

"Ni kweli nimefunza klabu kubwa," amesema, "Mipango ya Paris St-Germain ilikwa mizuri. Naamini itakuwa hivyo na hapa pia.

Nimeenda uwanja wa mazoezi jana. Mambo yalikuwa mazuri.

Mipango ya klabu kujenga uwanja mpya inaonesha kuwa klabu inataka mafanikio.

"Kukusanya mapato ni jambo kubwa katika mpira wa kisasa. Everton wanataka uwanja wao mpya ili uwasaidie kukusanya mapato na kuwa na ushindani mkubwa.

"Kwangu, itakuwa ni jambo zuri kuwepo hapa wakati uwanja mpya ukifunguliwa."