Bukayo Saka: Mchezaji wa Arsenal yupo njia panda kuhusu timu atakayoiwakilisha kati ya Nigeria na England

Bukayo Saka

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kinda na winga wa Arsenal Bukayo Saka

Winga wa Arsenal Bukayo Saka, ambaye anaweza kuichezea England au Nigeria amesema kwamba anafikiria kuhusu ni timu gani ambayo anataka kuiwakilisha kimataifa na kwamba hatofanya uamuzi wa haraka.

''Mimi huwa nafikiria mara kwa mara lakini bado sijapata uamuzi'' , mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 aliambia BBC Sport.

Saka ambaye ni mzaliwa wa wazazi Wanigeria ameiwakilisha England katika mechi za vijana.

Pia unaweza kusoma:

Mchezaji huyo aliyefuzu kutoka shule ya mafunzo ya soka ya Arsenal amesema kwamba kati ya mataifa hayo mawili hakuna hata moja ambalo limewasilisha ombi lao kwake kuchezea timu yake ya taifa.

''Hakuna mtu ambaye amewasiliana nami lakini nitakapofanya uamuzi mutajua'', alisema Saka.

Winga huyo mwenye kipaji anaendelea vyema na Arsenal.

Alianza kushiriki katika mechi za ligi kuu ya Premia akiwa na umri wa miaka 17 - akiweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza aliyezaliwa 2001 kushiriki katika ligi ya Premia.

Mchezaji huyo alimpongeza aliyekuwa mkufunzi wa Arsenal Unai Emery kwa kumpatia fursa .

''Namshukuru sana kwasababu alikuwa na matumaini mengi kutoka kwangu , alinichezesha kwa mara ya kwanza na akaendelea kunisukuma . Nitamshukuru maisha yangu yote. Ni kitu ambacho kimekuwa ndoto yangu , kutoka katika shule ya mafunzo na kuingia katika kikosi cha kwanza cha Arsenal''.

Kwa sasa Saka anasema kwamba anatazama hatma yake na mkufunzi mpya wa Arsenal Mikel Arteta.

''Nimesikia vitu vya kutia moyo kutoka kwake na niko tayari kufanya kazi naye''.