'Unyonge wa Liverpool kwa miaka 30 EPL umefikia kikomo'

Jordan Henderson, Trent Alexander-Arnold and Andy Robertson

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kipigo cha 4-0 didi ya Leicester ilikuwa ni ishara tosha kuwa LIverpool haitanii msimu huu.

Japo wenyewe hawasemi, ama yawezekana hawataki kunukuliwa wakisema, miaka 30 ya kushindwa kuchukua taji la Ligi ya Primia kwa Liverpool hatimaye inaelekea kufika kikomo.

Hawawezi kusema hadharani, ama kuonesha furaha yao kwa sasa, kwa kuwa katika miaka hiyo 30 kumekuwa na vipindi ambavyo walikaribia kunyakua kombe lakini likawaponyoka.

Lakini yaonekana mwaka huu hadithi ni tofauti, ubora wa kikosi ni wa hali ya juu, yawezekana ikawa sahihi kusema kikosi hiki cha sasa ndiyo bora zaidi kuliko vyote katika miongo mitatu iliyopita.

Nuru ya ushindi iling'ara zaidi kwa vijana hao wanaonolewa na Mjerumani Jurgen Klopp baada ya kuichapa Leicester City inayoshika nafasi ya pili kwa goli 4-0 siku ya Boxing Day.

Ushindi wa Liverpool uliambatana na kiwango safi cha umiliki wa kandanda, Leicester ambayo watu walikuwa wakiipigia chapuo la kuizuia Liverpool na kufanya maajabu ya kuchukua ubingwa kama mwaka 2016 walikuwa zaidi ya wanyonge katika mchezo huo uliopigwa dimbani kwao.

Kwa matokeo hayo, Liverpool ikafikisha alama 52, na kuifanya ikae kwenye usukani wa ligi kwa tofauti ya alama 13 dhidi ya Leicester yenye alama 39.

Ijumaa Disemba 27, ikawa siku njema pia kwa Liverpool japo hawakushuka dimbani, mabingwa watetezi Manchester City ambao wapo nafasi ya tatu wakapoteza mchezo wao dhidi ya Wolves kwa goli 3-2.

Kwa matokeo hayo, pengo baina ya Livepool na Man City yenye alama 38 ni pointi 14.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Pep Guardiola akiri kuwa Man City haiwezi kuifikia kasi ya Liverpool msimu huu

Ikumbukwe pia kuwa Livepool ana mchezo mmoja mkononi hivyo endapo ataushinda mchezo huo atakuwa na alama 55.

Baada ya mchezo dhidi ya Wolves, kocha wa Man City Pep Guardiola alikiri kuwa safari ya ubingwa kwao imefikia tamati.

"Pengo ni kubwa sana...ni kitu kisicho na uhalisia kwa sisi kuanza kuwafikiria Liverpool. Kwa sasa tunawapigia hesabu Leicester, tunaamini tunaweza kurudi katika nafasi ya pili," amesema Guardiola.

Kwa upande wa kocha wa Leicester, Brendan Rodgers pia itakuwa ni vigumu sana kuwazuia Liverpool.

"(Liverpool) Ni timu nzuri sana. Kiwango chao cha kujiamini kipo juu. Wamekuwa ni wazoefu wa kushinda na hawajapoteza michezo mingi katika miezi 18 iliyopita. Sasa wana wachezaji wa kutosha, uzoefu na ubora wa kuwafanya wamalize kazi mapema."

Klopp: Hakuna kilichoamuliwa

Kocha wa Liverpool kwa upande wake anaonekana kukagua kila neno analoliongea kuhusu mustakabali wa ubingwa.

Naam, uhalisia ni kuwa bado kuna mechi 20 zinawasubiri kabla ya kumaliza msimu huu.

Nusu yao ya ligi, sawa na michezo 19 itakuwa kesho dhidi ya Wolves. Mpaka sasa Liverpool wameshinda mechi 17 na kutoka sare mchezo mmoja tu dhidi ya mahasimu wao Man United.

"Bado hakuna chochote kilichoamuliwa, sisikii maamuzi yeyote kwenye masikio yangu. Sisi tunajitahidi kufanya kila tuliwezalo kujiandaa na mechi zetu zinazofuata," anadai Klopp.

Maelezo ya picha,

Klopp: Mipango yetu ni kujiandaa na michezo yetu ijayo

Licha ya kauli hiyo ya Klopp, uhalisia ni kuwapengo baina yao na timu zinazowafukuza katika msimamo wa ligi ni kubwa.

Si jambo linaloyumkinika kuona Liverpool ambayo haijafungwa michezo ya ligi 34 iliyopita kudondosha alama 14 mpaka msimu utakapokamilika mwakani.

Toka mwaka 2019 uanze Livepool imefungwa mchezo mmoja tu wa ligi.

Ili ubingwa uwaponyoke msimu huu, basi watalazimika kufungwa michezo mitano kati ya 20 ijayo, huku wapinzani wao wa karibu, Man City na Leicester washinde michezo yao yote. Hakika hizo zitakuwa hesabu ngumu kutimia.

Mpaka sasa Man City washapoteza mechi tano kati ya 19 (mzunguko wa kwanza wa ligi). Msimu uliopita walipoteza mechi nne katika mechi zote 38.

Uongozi huu wa ligi wa Liverpool, kwa alam nyingi kama hizo kufikia siku ya 'Boxing Day' mara ya mwisho ulishikiliwa na Manchester United miaka 26 iliyopita msimu wa 1993-1994, ambapo United walinyakua ubingwa.

Kwa namna yeyote ile, Liverpool ni bingwa mteule wa ligi ya Primia msimu wa 2019/2020.

Mara yao ya mwisho kuchua taji hilo ilikuwa ni miaka 30 kamili iliyopita, msimu wa 1989/1990.