Mwanariadha maarufu awaonyesha kivumbi maafisa wa kukabiliana na dawa za kusisimua misuli Kenya

Baadhi ya wanariadha wamefeli vipimo vya dawa za kusisimua misuli na kupigwa marufuku katika mchezo huo
Image caption Mwanariadha awaonyesha kivumbi maafisa wa kukabiliana na dawa za kusisimua misuli Kenya

Mwanariadha maarufu nchini Kenya ametoroka kambini kwa lengo la kukwepa maafisa wa shirika la kukabiliana na dawa za kusisimua misuli ambao walikuwa wamemtembelea ili kumfanyia vipimo.

Kisa hicho kinaangazia changmoto ambazo shirika hilo linakabiliana nazo katika kuusafisha mchezo huo.

Katika kipindi cha miaka mitano iliopita , takriban wanariadha 60 wa Kenya wamewekewa vikwazo kwa kukiuka sheria za kukabiliana na dawa za kusisimua misuli.

Kundi hilo la maafisa wa shirika hilo liliwasili kisiri katika kambi hiyo ya Kapsabet iliopo magharibi mwa Kenya.

Baada ya kubaini wageni hao walikuwa maafisa wa kukabiliana na dawa hizo, mwanariadha huyo aliruka kupitia dirisha moja na baadaye kupita uwa ambalo lilikuwa limezunguka kambi hiyo - kwa haraka zaidi.

Barnaba korir wa shirika la Riadha nchini Kenya alithibitisha kisa hicho lakini hakutoa jina la mwanariadha huyo.

Mwanariadha huyo anatarajiwa kuadhibiwa .

Bwana Koris alisema kwamba wanariadha ambao wanajua kwamba wana hatia huona hawana njia nyengine isipokuwa kuwatoroka maafisa hao.

Katika kipindi cha juma moja lililopita, wanariadha wawili akiwemo Alfred Kipketer- bingwa wa dunia miongoni mwa wanariadha wachanga wasiozidi umri wa miaka 20 anayekimbia mbio za mita 800 wamesimamishwa kwa kukiuka sheria za kukabiliana na dawa hizo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii