Mabondia Deontay Wilder na Tyson Fury kuzipiga Las Vegas.

  • Na John Nene
  • BBC News Swahili
Deontay Wilder (l) and Tyson Fury

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Tyson Fury (kulia) Deontay Wilder (kushoto) wote hawajawahi kupoteza pambano

Gumzo limekua likiendelea juu ya ndondi kati ya bingwa wa uzani wa heavy mkanda wa WBC Deontay Wilder na mpinzani wake Tyson Fury watakapombana huko Las Vegas, Marekani tarehe 22 mwezi wa Februari, lakini je ni nani atakayeibusu sakafu kabla ya mwenzake?

Mabondia hao walienda sare katika pigano lao la kwanza mwaka wa 2018 huku Fury akilalamika waaamuzi waliegemea upande wa Wilder ambaye alimrambisha sakafu Fury raundi ya kumi lakini akamaliza raundi zote kumi na mbili.

Fury anasema atamuamgusha Wilder raundi ya pili.

``Nitaingia ulingoni nikiwa mzito kumshinda kwa hivyo makonde yake hayatanibabaisha kamwe, nitamshinda kwa KO raundi ya pili sicheki na mtu mie,'' anasema Fury.

Wilder hatahivyo haonyeshi mshangao wowote kwa vitisho vya Fury.

``Kama atashinda kwa KO raundi ya pili anavyosema basi nitastaafu kwa ndondi za kulipwa, ``anasema Wilder ambaye kama Fury hajapoteza hata pigano moja. Wilder ameshinda mapigano 42 akaenda sare mara moja na ameshinda mapigano 41 kwa KO. Fury naye ameshinda mara 29 na akaenda sare moja akiwa na KO 20..

Kwa upande wa mapato, Wilder na Fury wataweka kibindoni zaidi ya dola milion 28 na fedha zingine za kando za mapato ya televisheni. Haya ndiyo malipo yao ya juu zaidi tangu waanze kucheza ndondi za kulipwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kumekua na vita vya maneno kati yao

Vita vyao vya maneno viliendelea wakati wa kupima uzani huku Wilder akimwambia Fury kwamba ni yeye amemsaidia kupata malipo ya juu zaidi.

``Mimi nalisha familia yako kwa sababu ya wewe kucheza na mimi kama bingwa wa WBC,`` alifoka Wilder huku akiwa na mkanda wake begani.

Akimnyooshea kidole, Fury alimwambia Wilder ataona cha mtema kuni katika pigano lao la pili akisema sasa amebadilisha mbinu na atashambulia zaidi.

Wilder amepuuza yote hayo akisema:`` Hana nguvu huyu ni mdomo tu kwa sababu yeye ni mzito zaidi yangu. Ni bondia mzuri lakini makonde yake hafifu hayawezi kuniumiza mimi,'' anasema Wilder ambaye alikuwa na uzito wa 231lbs na Fury 273 lbs walipopimwa.

``Sioni ajabu kwa uzito wangu. Kwa familia yetu sote tumenenepa kuanzia baba yangu, mama na ndugu zangu wa kiume. Yetu ni familia ya watu walionenepa,'' alisema Fury mwenye umri wa miaka 31 naye Wilder ana umri wa miaka 34.

Kutokana na hasira zao, mabondia hao hawakuruhusiwa kukaribiana wakati wa kupimwa uzani. Walirushiana maneno kwa mbali huyku walinzi wakiwa katikati yao kudumisha usalama maanake walioneka wako tayari kuzipiga kavu kavu kila mmoja akitaka kuonyesha nani dume zaidi ya mwingine..

Kwa kawaida Wilder hutegemea sana konde lake la kulia kuwapeleka wapinzani wake usingizini. Si mwepesi sana kama Fury ambaye ana kasi zaidi ya Wilder. Wadadisi wa ndondi wanasema endapo pigano hilo litaendelea mpaka raundi ya pili Fury ana uwezo wa kuibuka mshindi kwa pointi lakini itabidi awe macho kabisa kuona konde la kulia la Wilder ambalo hutoka kama umeme na lina nguvu mno.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Deontay Wilder

Gwiji wa ndondi Mike Tyson anamshabikia wajina wake dhidi ya mmarekani mwenzake.

"Kila mara ninamshabikia kwasababu alipewa jina langu ," aliiambia BT Spot.

Lakini bingwa wa dunia David Haye hamuungi mkono muingereza mwenzake, ambapo aliliambia jarida la Express kwamba anatarajia Wilder atamaliza akiwa wa kwanza.

Na promota Eddie Hearn aliiambia IFL TV kwamba anaenendelea kubadili mawazo yake mara kwa mara ingawa (wakati anaandika ) anadhani Wilder atashikilia mkanda wake WBC.

THakuna mtu wa wazi ninayemshabikia zaidi na ndio maana huu ni mpambano mkali unaosubiriwa kwa hamu zaidi wa uzani mzito katika miaka ya hivi karibuni.

Fury binafsi alibashiri nock-out katika mzunguko wa pili. Hakuna mengi unayoweza kupata kutoka katika rekoti yake , au kutoka kwenye mpambano wake wa awali T, hilo linaashiria kuwa itatokea. Wengi wa mashabiki wanadhani kuwa ni suala la Fury kupitia kwa point na Wilder kupitia nock-out...