Deontay Wilder: Bondia wa Marekani alaumu vazi aliloingia nalo ulingoni kama sababu ya kushindwa na Tyson Fury

Vazi la Deontay Wilder

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Deontay Wilder alisema vazi lake liliadhimisha mwezi wa historia ya watu weusi

Bondia wa Marekani Deontay Wilder amelaumu vazi alilovaa na kuingia nalo ndani ya ulingo wa ndondi kama sababu iliomfanya kupoteza taji lake la WBC katika uzani mzito zaidi duniani kwa Muingereza Tyson Fury.

Raia huyo wa Marekani mwenye umri wa miaka 34 alisema kwamba vazi hilo lilikuwa zito sana hatua iliomfanya kukosa nguvu miguuni katika pigano hilo.

Fury mwenye umri wa miaka 34 alionyesha umahiri wake ili kushinda taji katika mji wa Las Vegas siku ya Jumamosi wakati kona ya Wilder iliposalimu amri kwa kutupa kitambaa cheupe wakati pigano hilo lilipokuwa limefika raundi ya saba.

Wilder pia aliambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba ataheshimu kifungo cha pigano la tatu la marudio dhidi ya Fury.

Fury hakuniumiza hata kidogo, lakini ukweli ni kwamba vazi nililovaa lilikuwa na uzito wa kilo 18.1 na ulikuwa mwezi wa kumbukumbu wa historia ya watu weusi.

Fury alibebwa kati ulingo wa ndondi kwa kujtumia kiti cha enzi na pia alikuwa amevalia taji la mfalme.

''Miguu yangu haikuwa na nguvu kuanzia mwanzo wa pigano, na katika raundi ya tatu miguu yangu ilikosa nguvu katika kipindi chote'', aliogezea Wilder.

''Nilivaa vazi hilo kwa mara ya kwanza usiku kabla ya pigano lakini sikudhania kwamba litakuwa na uzito wote huo''.

''Nilitaka vazi hilo liwe zuri na nadhani napatia hicho kipaumbele zaidi ya chochote kile''.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Fury alibebwa hadi katika ulingo wa ndondi kupitia kiti cha enzi

Fury alimshinda Wilder kwa konde moja zito na mchanganyiko wa ngumi za kulia katika raundi ya tatu kabla ya ngumi ya kushoto mwilini kumuangusha Wilder ambaye alikuwa hajapigwa katika raundi ya tano.

Wilder alikimbizwa hospitalini baada ya pigano lakini alisema kwamba hakupatwa na mshtuko ,kujeruhiwa ndani ya sikio ama hata kuvunjwa taya kama ilivyodaiwa , licha ya kuhitaji uuguzi kufunga jeraha katika sikio lake.

Pia alimkosoa naibu mkufunzi wake Mark Breland kwa kusitisha pigano hilo.

''Nimekerwa na Mark kwa sababu tumezungumza kuhusu hilo mara kadhaa kabla ya hili kutokea. Nilisema kama bingwa , kama kiongozi nataka kwenda kulinda hadhi yangu''.

''Hivyobasi niliambia timu yangu kwamba kutorusha taweli ulingoni kwa sababu mimi ni mtu maalum. Bado nimesalia na raundi tano licha ya chochote kile bado nilikuwa katika pigano''.

''Naelewa kwamba alikuwa akinijali na kujaribu kufanya kile ambacho alihisi kilikuwa sawa, lakini haya ni maisha yangu na kazi yangu na lazima akubali ombi langu''.

Wilder ana takriban siku 30 kufutilia mbali kifungo cha kandarasi cha marudio ya piganpo hilo ili kujaribu kulikomboa taji lake kutoka kwa Fury , baada ya kutoka sare katika pigano lao la kwanza Disemba 2018.