Coronavirus: Freeman Mbowe asema mtoto wake ameambukizwa virusi vya corona ndani ya Tanzania

Freeman Mbowe Haki miliki ya picha Freeman Mbowe/Instagram
Image caption Freeman Mbowe amekiri mtoto wake kukutwa na virusi vya corona

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe amekiri mtoto wake kubainika na virusi vya corona na kueleza kuwa amepata maambukizi hayo bila kusafiri nje ya nchi.

Katika taarifa yake kwa umma, Mbowe amesema kuwa mtoto wake aitwaye Dudley amethibitika kupatikana na virusi vya Corona baada ya kupata homa za vipindi, kuumwa kichwa mfululizo na kukohoa kwa siku tano.

"Hali ya Dudley sasa imeimarika. Homa zimekwisha. Kichwa kimepona. Bado anakohoa kiasi na yuko chini ya uangalizi maalum kwenye 'isolation'," amesema Mbowe na kuongeza: "Dudley hajasafiri nje ya nchi mwaka huu. Maambukizi haya kayapata ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam."

Mbowe ametoa taarifa yake Jumanne jioni baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, kutangaza awali kuwa mtoto wa kiongozi huyo amepata maambukizi.

"Mama yake, ambaye ni Daktari alipobaini hali hiyo alizitaarifu mamlaka za Serikali zinazoshughulikia Janga hili nazo zilimtaka kijana apelekwe Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam kwenye vipimo zaidi ambapo ilithibitika rasmi kuwa ana virusi vya corona.

Huwezi kusikiliza tena
Coronavirus: Kila mgeni atakayeingia Tanzania kufikishwa karantini

"Aidha, timu ya Serikali imeendelea kutoa ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu kwa familia yote ikiwemo ushauri nasaha kwa wanafamilia na marafiki wengine waliokutana na Dudley katika mikusanyiko mbalimbali ikiwemo kuweka wengine in Isolation au karantini," ameeleza Mbowe.

"Siyo wakati wa kulumbana"

Kumekuwa na kupishana kwa maoni juu ya hatua za kuchukuliwa katika kudhibiti virusi vya corona nchini Tanzania huku baadhi ya wapinzani wakikosoa mipango ya serikali.

Jana, Makonda aliwashambulia baadhi ya wanasiasa hao akiwemo Mbowe na Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe kuwa wamefilisika kisiasa.

"Wengi wako tayari kukusaidia. Chadema tuko tayari kukusaidia na kulisaidia Taifa. Siyo wakati wa kulumbana huu," ameeleza na kuongeza, "Hatustahili kuchefuliwa na kejeli za Paul Makonda kipindi hiki. Tusiiachie serikali pekee. Tutajuta. Tusiilaumu tu, tuishauri nayo iwe tayari kuupokea ushauri na ishirikishe. Ni janga la Dunia na hakika tutaumizwa kuliko tunavyowaza."

Kwa mujibu wa Mbowe, njia mojawapo muhimu ya kulishinda tatizo ni kulikubali na kulikabili kwa nguvu zote na kwa umoja.

"Rai kwa Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli: Unda timu ya kukusaidia na ushirikishe wadau wengine nje ya Serikali yako. Yako mengi ya kufanya nje ya mikakati ya kitabibu inayosimamiwa na Waziri Mkuu na Waziri Ummy Mwalimu. Katika maisha maandalizi hayajawahi kuwa hasara, bali hasara iliyo."

Wagonjwa 12 wathibitishwa Tanzania

Haki miliki ya picha IKULU TANZANIA
Image caption Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli

Siku ya Jumapili Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ametangaza kuwa nchi hiyo ina wagonjwa 12 walioambukizwa ugonjwa wa corona.

Wanane kati ya wagonjwa hao ni raia wa Tanzania na wengine wanne ni raia wa kigeni.

Nchi hiyo imechukua hatua kadhaa za kudhibiti maambulikzi ikiwemo kufunga shule na vyuo vikuu na kuzuia wananchi kuwa katika mikusanyiko isiyo ya lazima.

Pia kuanzia jana Jumanne, watu wote watakaongia nchini humo watatakiwa kukaa chini ya uangalizi maalumu 'isolation' kwa kipindi cha wiki nne kwa gharama zao binafsi.

Mada zinazohusiana