Mesut Ozil: Hatima ya kiungo mshambuliaji wa Arsenal haijulikani

Ozil alijiunga na washika bunduki mwaka 2013

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Ozil

Kiungo wa Arsenal Mesut Ozil ameachwa nje kwenye kikosi cha Arsenal kitakachoshiriki kombe la Europa kwa ajili ya kampeni zijazo.

Hatima ya mchezaji huyo wa miaka 31 katika klabu hiyo bado haijulikani baada ya kutemwa na mkufunzi Mikel Arteta.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani hajaichezea Gunners tangu mwezi Machi.

Thomas Partey aliyesajiliwa kwa pauni milioni 45 kutoka klabu ya Atletico Madrid amejumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 kabla ya mechi yao ya kwanza ya kundi B dhidi ya klabu ya Rapid Vienna baadae tarehe 22 mwezi Oktoba.

Washika bunduki hao pia watakutana na Dundalk ya Ireland na Molde ya Norway katika hatua ya makundi.

Siku ya Jumanne, Ozil, ambaye alijiunga na klabu kwa rekodi ya pauni milioni 42.4 mwaka 2013 na ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, alisema atamlipa mshahara mtu anayevaa kikaragosi cha mascot kuburudisha mashabiki wa Arsenal uwanjani, kabla na baada ya mechi.

Vilevile wachezaji wawili wa Arsenal Sokratis Papastathopoulos na William Saliba hawajaorodhoreshwa katika kikosi hicho cha wachezaji 25.