Je, nchi za Afrika Mashariki kutikisa tena Afcon?

African Cup of Nations

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON)

Mwaka 2019 Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) liliweka rekodi ya kuwakilishwa na idadi kubwa ya timu katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizofanyika huko Misri.

Timu nne za Taifa kutoka ukanda huu zilifuzu kushiriki fainali hizo ambazo timu ya taifa ya Algeria ilitwaa ubingwa kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Senegal ambazo ni timu za taifa za Tanzania 'Taifa Stars', Kenya 'Harambee Stars', Uganda 'The Cranes' na Burundi 'Intamba' ziliweza kushiriki fainali hizo idadi ambayo ni kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Kabla ya hapo, idadi kubwa ya timu zilizo chini ya CECAFA kushiriki kwa pamoja katika Fainali za AFCON ilikuwa ni tatu ambapo ilikuwa ni mwaka 1976, pindi ilipowakilishwa na timu za taifa za Ethiopia waliokuwa wenyeji wa fainali hizo, Sudan na Uganda.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Katika mchuano wa kombe la Cecafa mwaka 2013: Sudan ikiwa uwanjani na Rwanda

Mwaka 2004, CECAFA angalau ilitaka kujitutumua lakini ikaishia kuwakilishwa na timu mbili tu katika mashindano hayo yaliyofanyika Tunisia ambapo bendera yake ilipeperushwa na timu za Kenya na Rwanda.

Baada ya kile kilichofanyika mwaka juzi, wengi walitegemea kuona hiyo ndio itakuwa mwanzo wa nchi wanachama wa CECAFA kuanza kutikisa soka la Afrika na kuwakilishwa na idadi kama ya mwaka juzi ya timu au zaidi ya hapo kama ishara ya kuonyesha kuimarika kwa timu za taifa kutoka ukanda huu.

Hata hivyo msimamo wa makundi ya mashindano ya kuwania kufuzu awamu ijayo ya AFCON lakini pia aina ya mechi na ushindani ulio mbele ya timu za taifa zilizo chini ya CECAFA havitoi imani kubwa kwamba wanaweza kurudia kile walichokifanya 2019 tofauti na wengi walivyoamini kabla harakati hizo za kuwania kufuzu hazijaanza.

Wakati timu tano zikiwa zimeshajihakikishia tiketi ya kushiriki AFCON mwakani ambazo ni wenyeji Cameroon, Mali, Algeria, Senegal na Tunisia, bado hakuna timu kutoka ukanda wa CECAFA iliyo na uhakika wa kufuzu fainali hizo hadi sasa kulingana na msimamo wa kundi ambalo kila moja ipo na nyingi zinategemea upepo wa bahati ili angalau ziweze kufuzu jambo linaloleta wasiwasi kwamba huenda safari hii kukawa na idadi ndogo ya timu zitakazowakilisha Afrika Mashariki na Kati katika fainali za AFCON.

Ikumbukwe katika mashindano haya ya kuwania kufuzu Fainali za AFCON, CECAFA inawakilishwa na timu nane ambazo zimepangwa katika makundi tofauti na ni timu tatu tu kati ya wanachama wake 11 wanaoshiriki mashindano ya CAF kwa timu za taifa ambazo hazikupata fursa ya kuwepo katika hatua ya makundi ambazo ni Somalia, Eritrea na Djibout.

Timu nane kutoka CECAFA zilizopo katika hatua ya makundi ni Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

Makala hii inakuangazia nafasi ya kila timu kutoka CECAFA katika kusaka tiketi ya kushiriki AFCON na ni kwa namna gani zinaweza kufanya ili ziweze ama kurudia au kufanya zaidi ya kile kilichotokea mwaka 2019.

Burundi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Timu ya taifa ya Burundi

Fainali za AFCON za mwaka 2019 zilikuwa za kwanza kwa taifa hilo kushiriki na ilimaliza ikiwa imeshika mkia katika kundi B lililokuwa na timu za Madagascar, Nigeria na Guinea ambapo haikufunga bao hata moja.

Katika mashindano ya kufuzu awamu ijayo ya AFCON, Burundi ilipangwa katika kundi E lenye timu za Morocco, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mauritania.

Ikiwa nafasi ya tatu kwenye kundi hilo na pointi zake nne, nafasi ya Burundi kufuzu kwa mara ya pili mfululizo AFCON itapatikana ikiwa tu wataibuka na ushindi katika mechi zake mbili dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati watakaocheza nyumbani, Machi 26 na ule wa ugenini dhidi ya Morocco, Machi 30.

Kinyume na hapo italazimika kutegemea zaidi matokeo ya washindani wake wawili wakubwa kwenye kundi hilo, Morocco na Mauritania kuona kama inaweza kujihakikishia tiketi ya kushiriki fainali za Afrika.

Morocco inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi 10, inahitaji pointi moja tu ili ikate rasmi tiketi ya kushiriki AFCON wakati Mauritania iliyo katika nafasi ya pili na pointi tano, inahitajika kushinda mechi yake dhidi ya Morocco, Machi 26 na kuombea Burundi ipoteze dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ili nayo ifuzu.

Ethiopia

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Timu ya taifa ya Ethiopia

Utofauti mdogo wa pointi uliopo baina ya timu tatu za juu kwenye kundi K, unaiweka Ethiopia katika matumaini makubwa ya kufuzu fainali zijazo za AFCON ikiwa itachanga vyema karata zake katika mechi mbili zijazo dhidi ya Madagascar nyumbani na ile ya ugenini dhidi ya Ivory Coast.

Ushindi katika mechi hizo mbili utaihakikishia Ethiopia tiketi ya kushiriki AFCON lakini pia hata isiposhinda zote inaweza kufuzu ikiwa itapata ushindi wa kuanzia mabao 2-0 dhidi ya Madagascar na kisha kutoka sare ugenini na Ethiopia.

Kwa sasa kundi hilo linaongozwa na Ivory Coast yenye pointi saba sawa na Madagascar iliyo katika nafasi ya pili, Ethiopia inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita wakati Niger inashika mkia ikiwa na pointi tatu.

Kama Ethiopia itapoteza mechi ijayo nyumbani dhidi ya Madagascar, Machi 26 na Ivory Coast ikashinda dhidi ya Niger, Ethiopia itakuwa imekosa rasmi tiketi ya kushiriki fainali zijazo za AFCON.

Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kenya

Matokeo yoyote tofauti na ushindi katika mechi mbili zilizobakia za timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' dhidi ya Misri na Togo, yataifanya ikose tiketi ya kushiriki fainali zijazo za mataifa ya Afrika.

Harambee Stars inayonolewa na kocha Jacob 'Ghost' Mulee inahitajika kupata ushindi dhidi ya Misri nyumbani, Macho 25 na dhidi ya Togo ugenini Machi 29 na kisha kuomba Misri na Comoro zenye pointi nane kila moja kufanya vibaya katika mechi zao zilizosalia ili yenyewe iweze kufuzu.

Lakini pia hata kama itashinda mechi zake mbili zilizobakia, Kenya inaweza isifuzu ikiwa Misri na Comoro kila moja itapata angalau pointi mbili tu kwenye mechi zao mbili zilizobakia.

Sudan

Sudan ipo katika kundi C ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake sita, Ghana inaongoza ikiwa na pointi tisa sawa na Afrika Kusini wakati Sa Tome na Principe wanashika mkia wakiwa hawana pointi.

Ushindi katika mechi mbili zijazo, dhidi ya Sao Tome na Principe ugenini na mbele ya Afrika Kusini nyumbani, utaifanya ifikishe pointi na kuweza kufuzu ikiwa itaifunga Afrika Kusini kwa mabao kuanzia 2-0.

Kinyume na hapo wanaweza kujikuta katika nafasi ngumu ya kufuzu AFCON.

Sudan Kusini

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mashabiki wa soka Sudan Kusini

Sudan Kusini inashika mkia kwenye kundi B ikiwa na pointi tatu, Burkina Faso ikiwa inaongoza na pointi zake nane, Uganda inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi saba na Malawi yenye pointi nne.

Ushindi wa aina yoyote ambao Burkina Faso na Uganda zitapata katika mechi moja tu kati ya mbili ambazo kila moja imebakisha utamaanisha kuwa Sudan Kusini imekosa rasmi tiketi ya kushiriki AFCON kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Uganda

Maelezo ya picha,

Uganda Cranes

Kati ya nchi nane za Afrika Mashariki na Kati, Uganda ndio wako kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufuzu AFCON kwani wanahitaji ushindi angalau katika mechi moja tu kati ya mbili walizobakiza ili watimize lengo hilo.

Timu hiyo inayonolewa na kocha Abdallah Mubiru ina mechi moja nyumbani dhidi ya Burkina Faso itakayochezwa Machi 24 na baada ya hapo itakuwa na kibarua ugenini dhidi ya Malawi, Machi 29.

Kama itafuzu, Uganda itakuwa inafanya hivyo kwa mara ya nne mfululizo.

Rwanda

Ikiwa inashika mkia kwenye kundi F na pointi zake mbili, ni miujiza tu inayoweza kuifanya Rwanda ifuzu fainali zijazo za AFCON.

Tayari Cameroon ineshachukua nafasi moja kwenye kundi ya kufuzu AFCON kupitia kundi hilo baada ya kufikisha pointi 10 na nafasi moja iliyobaki inawaniwa na Cape Verde na Msumbiji zenye pointi nne kila moja na Rwanda iliyo na pointi mbili.

Rwanda inahitajika kupata ushindi katika mechi zake mbili zilizobakia, ile ya tarehe 24, Machi nyumbani dhidi ya Msumbiji na pia ya Machi 30 ugenini dhidi ya Cameroon na kisha kuziombea Cape Verde na Msumbiji zifanye vibaya ili yenyewe iweze kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika zijazo.

Tanzania

Timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' nayo ipo katika nafasi ngumu ya kufuzu AFCON kupitia kundi J lenye timu za Tunisia, Libya, Tanzania na Guinea ya Ikweta.

Tunisia yenye pointi 10 tayari imeshajihakikishia tiketi yake na sasa kuna nafasi moja pekee katika kundi hilo inayowaniwa na Tanzania, Guinea ya Ikweta na Libya.

Mchezo wa ugenini dhidi ya Guinea ya Ikweta, Machi 25 umeshikilia kwa kiasi kikubwa hatima ya Taifa Stars kushiriki fainali zijazo za AFCON.

Ushindi utaifanya ifikishe pointi saba na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo na hivyo kuhitajika kushinda mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya Libya, Machi 29 ili ifuzu.

Ikiwa itapoteza, itakosa rasmi tiketi ya kucheza AFCON na iwapo itatoka sare italazimika kuombea Guinea ya Ikweta ipoteze mechi ya mwisho dhidi ya Tunisia na yenyewe ishinde dhidi ya Libya ili ifuzu.