Lionel Messi: PSG inadaiwa kuchunguza kinachoendelea kati ya Barcelona na mchezaji huyo

Ronald Koeman na Lionel Messi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Lionel Messi na Ronald Koeman

Barcelona haijaanza mazungumzo ya kutia saini kandarasi mpya na Lionel Messi na PSG inafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea kulingana na mtaalamu wa soka nchini Uhispania Guillem Balague.

Mkataba wa mshambuliaji huyo wa Argentina 33, unakamilika mwisho wa msimu huu na bado hajakubali kandarasi mpya.

Baadhi ya wachezaji huenda wakaondoka katika klabu hiyo ya La Liga katika kipindi cha miezi kadhaa ijayo.

''''Messi ataangalia wiki mbili zijazo wakati uamuzi utakapofanyika , Ballague amesema.

Messi alituma ujumbe Barcelona mwezi Agosti 2020 akisema kwamba alitaka kutumia kifungu cha sheria ya kandarasi yake ambayo alisema inaweza kumruhusu kuondoka kwa uhamisho wa bila malipo.

Lakini klabu hiyo ilisema kwamba kitita cha Yuro milioni 700 katika kifungu cha sheria ya kumuachia ni sharti kiafikiwe.

Alilazimika kusalia na mabingwa hao wa La Liga , akisema kwamba haiwezekani kwa mtu yeyote kulipa fedha kama hizo.

Messi alisema wakati huo kwamba hatua yake ya kutoiambia Barcelona kwamba angetaka kuondoka kabla ya Juni 10 ilikuwa muhimu, na iwapo angefanya hivyo , sheria ya kumuachilia isingemfunga.

Mkufunzi Ronald Koeman alisema kwamba anatumai Messi hakucheza mechi yake ya mwisho ya Barcelona katika uwanja wa Nou Camp kufuatia kushindwa nyumbaji na Celta Vigo kwa bao 2-1 siku ya Jumapili, lakini mshambuliaji huyo amepatiwa likizo na kwamba atakosa mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Eibar.

Kushindwa kwao kulivunja matumaini yao ya kushinda taji la ligi na kwamba ina maana watamaliza nje ya nafasi mbili bora za kwanza kwa mara ya kwanza tangu 2007-08.

''Atalazimika kuamua iwapo anataka kusalia katika klabu hiyo kwa misimu kadhaa wakati ambapo timu mpya inaanza kuundwa ama iwapo anataka kuisadia PSG kushinda mataji ya klabu bingwa'' , aliandika Balague katika mtandao wa twitter.

Hakuna mtu anayeweza kusema ataamua nini wakati huu.