Droo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya: Manchester City Kuvaana na PSG wakati Chelsea itajiuliza kwa Juventus.

Manchester City ikisherehekea ushindi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Man City iliichapa PSG mabao 4-1 kwa jumla katika mbili za nusu fainali ya michuano hyo msimu uliopita.

Mabingwa wa ligi kuu England Manchester City wamepangwa kundi moja na Paris St-Germain, RB Leipzig na Club Bruges katika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Ulaya.

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Chelsea yenyewe itakutana na wakali wa Serie A Juventus, Zenit St Petersburg ya Urusi na Malmo kutoka Sweden.

Manchester United wao wamepangwa kuvaana na Villarreal, ambao ni mabingwa wa ligi ya Europa baada ya kuwazaba Manchester United kwenye fainali msimu uliopita, pia wapo Atalanta ya Italia na Young Boys ya Switzerland.

Liverpool kwa upande wao wako kwenye kundi la kifo pamoja na timu za Atletico Madrid, Porto na AC Milan.

Droo kamili ya Makundi:

Kundi A: Manchester City, Paris St-Germain, RB Leipzig, Club Bruges

Kundi B: Atletico Madrid, Liverpool, Porto, AC Milan

Kundi C: Sporting Lisbon, Borussia Dortmund, Ajax, Besiktas

Kundi D: Inter Milan, Real Madrid, Shakhtar Donetsk, Sheriff Tiraspol

Kundi E: Bayern Munich, Barcelona, Benfica, Dynamo Kyiv

Kundi F: Villarreal, Manchester United, Atalanta, Young Boys

Kundi G: Lille, Sevilla, FC Salzburg, Wolfsburg

Kundi H: Chelsea, Juventus, Zenit St Petersburg, Malmo

Mchanganyiko kwa Vilabu vya Uingereza

Fainali ya Ligi ya mabingwa msimu huu itapigwa katika uwanja wa St Petersburg Stadium huko Urusi Jumamosi ya Mei 28.

Ni Droo yenye hisia mchanganyiko kwa Vilabu vya Uingereza

Kikosi cha Man City cha Pep Guardiola, ambacho kilichapwa na Chelsea katika fainali ya msimu uliopita, kinakutana na PSG yenye nyota mpya Lionel Messi aliyewahi kunolewa na Pep akiwa Barcelona kwenye kundi A.

Kingine cha kuvutia kwenye mechi za kundi hilo ni kwamba, huenda ikashuhudiwa Messi kukutana na hasimu wake wa muda mrefu kisoka Cristiano Ronaldo, aayehusishwa sana na mipango ya kuhamia Manchester City kutoka Juventus kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya pili mfululizo kwenye michuano hiyo baada ya msimu uliopita kukutana kwenye nusu fainali na City kushinda kwa jumla mabao 4-1.

Wakali wa Bundesliga RB Leipzig si wakuwadharau, wataleta upinzani wakiwa historia ya kuwaondosha Manchester United katika hatua ya makundi msimu uliopita.

Kikosi cha Jurgen Klopp na mabingwa mara sita wa michuano hiyo Liverpool wanatajwa kuwa kwenye kundi gumu na la kifo msimu huu, wakiwa na mabingwa wa La Liga Atletico Madrid, Porto ya Ureno mabingwa wa mwaka 1987 na 2004 - pamoja na bingwa mara saba wa michuano ya Ulaya AC Milan ya Italia.

Liverpool iliitandika Milan katika fainali maarufu ya ligi ya mabingwa ya 2005 huko Istanbul, Uturuki, lakini waitalia hao waliweza kulipiza kisasi miaka miwili baadae.

Kazi kubwa kwa kikosi cha Chelsea kinachonolewa na Thomas Tuchel' itakuwa mchezo wake wa nyumbani na ugenini dhidi ya Juventus, lakini hawatakuwa na kazi ngumu watakapokabiliana na na timu za Zenit na Malmo.

Ole Gunnar Solskjaer atakuwa mtu mwenye furaha kufuatia timu yake ya Manchester United kupewa nafasi kubwa kwa kusonga mbele kwenye kundi F, baada ya kuondolewa kwenye hatuaa ya makundi msimu uliopita.

Mashetani hao wekundi watakuwa na lengo la kulipiza kisasi dhidi ya Villareal inayonolewa na Unai Emery, baada ya kutandikwa kwa penati kwenye fainali ya ligi ya Europa msimu uliopita.