Manchester United yaafikiana makubaliano na Cristiano Ronaldo

Cristiano Ronaldo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Cristiano Ronaldo

Klabu ya Manchester United inafanya mazungumzo ya kumsaini nahodha wa timu ya taifa ya Portugal Christiano Ronaldo .

Mahasimu wao Manchester City wameamua kwamba hawatamfuatilia tena mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 baada ya kuangazia suala hilo kwa umakini.

Mkufunzi wa Juventus Massimiliano Allegri amethibitisha kwamba Ronaldo amesema kwamba hana hamu tena ya kuwachezea mabingwa hao wa Itali.

Mkufunzi wa United Ole Gunnar Solskjaer alisema kwamba Ronaldo "anajua kwamba tuko hapa '' wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa.

Ronaldo alisajiliwa na Manchester United kutoka Sporting Lisbon kwa dau la £12.2m mwaka 2003 na kufanikiwa kufunga magoli 118 katika mechi 292 akiichezea klabu hiyo..

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mapema siku ya Ijumaa , kabla ya habari za kumnyatia Ronaldo kubainika, Solskjaer alisema alishangazwa kwamba mshindi huyo mara tano wa taji la Ballon d'Or alitaka kusitisha huduma zake Itali.

Aliongezea kwamba Ronaldo alikuwa amewasiliana na kiungo wa kati wa United Bruno Fernandes, mchezaji mwenza wa timu ya Portugal.

"Sikufikiria Cristiano Ronaldo ataondoka Juventus'' , Solskjaer alisema. Kumekuwa na uvumi mapema leo na uvumu siku chache zilizopita.

"Najua Bruno amekuwa akizungumza naye pia. Anajua tunachohisi kumhusu na iwapo angetaka kuondoka Juventus anajua tuko hapa."

Manchester City ndio iliokuwa ikipigiwa upatu kumsajili mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid , wakati ripoti ziliposema kwamba tayari makubaliano yameafikiwa kati ya United na Ronaldo.

Akizungumza kabla ya City kucheza dhidi ya Arsenal katika ligi ya premia siku ya Jumamosi, mkufunzi Pep Guardiola alisema: "Cristiano ni mchezaji wa Juventus siwezi kuongeza chochote kile.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mkufunzi wa Man United Olegunar Solskjaer

"Katika siku hizi tatu au nne zilizosalia hadi kufungwa kwa dirisha la uhamisho , chochote kile kinaweza tokea, lakini kwa mtazamo wangu , kuna wachezaji wachache - Cristiano Ronaldo akiwemo , Messi ni mwengine - wanaamua kule ambako wataelekea kucheza'' .

''Hivi sasa , hisia zangu ni kwamba nimefurahi sana na kikosi tulichonacho na tutasalia tulivyo''.

Siku ya Jumatano, Juventus ilimwambia Ronaldo kwamba iko tayari kumuuza wakati wa dirisha la uhamisho lakini tu iwapo masharti yao yataafikiwa na klabu zinazomnyatia.

''Ronaldo alileta mchango wake na sasa ni wakati anaondoka na maisha lazima yaendelee'', Allegri alisema siku ya Ijumaa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mkufunzi wa Juventus Massimmiliano Allegri

''Mambo hubadilika, ni sheria za maisha. Juventus inasalia ambacho ndio kitu muhimu. Tunamshukuru kwa kile ambacho amekifanya , pia kama mfano miongoni mwa vijana .Lakini kama nilivyosema , lazime maisha yaendelee''.

Kulingana na ripoti , Ronaldo aliwaelezea wenzake wa Juventus kwamba anapanga kuondoka mwezi huu baada ya miaka miwili akiwachezea mabingwa hao wa Serie A.

Baadaye aliendesha gari lake hadi katika juwanja wa mazoezi siku ya Ijumaa asubuhi lakini akaondoka kabla ya kushiriki katika mazoezi hayo.

Wiki moja iliopita, Allegri alisema kwamba Ronaldo, hakuwahi kusema kwamba angependelea kuondoka Juventus na kwamba mchezaji huyo alikuwa amemwambia mkufunzi huyo kwamba atasalia katika uwanja wa Allianz Stadium.

Ronaldo mwenyewe alitaja uvumi wa vyombo vya habari kuhusu hatma yake ''kuwa ukosefu wa heshima kwake kama mtu binafsi katika chapisho refu la mtandao wa Instagram siku chache mapema.