KFF yapinga kutengwa katika soka Kenya

Mpira wa soka.
Image caption Usimamizi wa Kandanda umekuwa ukizua mvutano mkubwa nchini Kenya.

Katika mgogoro unaoendelea, shirikisho la soka la Kenya, KFF, baada ya kupoteza rufaa katika mahakama ya usuluhishi wa migogoro ya michezo, kutaka litambuliwe kusimamia soka ya Kenya, limesema halikubaliani na uamuzi unaonufaisha wapinzani wao, FKL.

Mahakama ya usuluhishi wa migogoro ya michezo, The Court of Arbitration for Sport (CAS), iliamua kuwa Football Kenya Limited (FKL) ndiyo itasimamia shughuli za soka nchini Kenya.

Lakini Kenya Football Federation (KFF) imesema haikubali na inapinga uamuzi huo. "Hatubaliani kabisa na uamuzi huu, tumeshangazwa sana," mwenyekiti wa KFF , Sam Nyamweya alieleza.

Shirikisho la soka la duniani Fifa linaitambua FKL kama mamlaka halali ya kusimamia soka ndani ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mgogoro baina ya pande hizo mbili umekuwa ukiunguruma kwa zaidi ya miaka sita.

"Endapo CAS inasema sisi siyo wanachama wa Fifa na hatukutakiwa kwenda CAS, basi walitakiwa kukataa kesi yetu tangu mwanzo," Bw Nwamweya alisema.

"Tunasubiri wanasheria wetu watushauri kuhusu hatua tunazoweza kuchukua na ninakuhakikishia kuwa tutachukua hatua."

Sheria

Sheria za CAS zilizochapishwa kwenye tovuti yake zinasema kuwa pande husika zinatakiwa kukubaliana na mchakato huo kwa maandishi.

Zinasema rufaa huruhusiwa tu kwa mazingira ya aina fulani, kukosekana kwa sheria, ukiukwaji wa taratibu au kutoshabihiana kwa sera za umma.'

Mkuu wa FKL, Mohamed Hatimy, anatumai uamuzi wa CAS utamaliza mgogoro huo.

"Ni matumaini yetu kuwa kupitia usuluhishi wa CAS, mgogoro huu wa muda mrefu hatimaye umepatiwa ufumbuzi wa kudumu," alisema.