Hatma ya Benitez Liverpool kujulikana

Meneja wa Liverpool Rafael Benitez wiki hii atakutana na Mwenyekiti wa klabu hiyo Martin Broughton huku kukiwa na uvumi wa yeye kuondoka Anfield.

Image caption Benitez kuzungumzia hatma yake Liverpool

Benitez, mwenye umri wa miaka 50, bado mkataba wake unamruhusu kuendela kuifundisha klabu hiyo kwa miaka minne ijayo, amekanusha taarifa zinazomhusisha kujiunga na klabu ya Juventus.

Amesema:"Ningependelea kuzungumzia zaidi soka. Mameneja hawawezi kujadili uvumi kila wakati".

Naye kiungo wa Liverpool Yossi Benayoun ameongezwa katika orodha ya walio mguu ndani mguu nje katika klabu hiyo na amekiri hana hakika na kuendelea kuchezea klabu hiyo.

Image caption Benayoun kuwepo kwake Livepool mashakani

Kufungwa mabao 2-0 siku ya Jumapili nyumbani na Chelsea kulimaliza matumaini ya Liverpool kumaliza nafasi nne ya Ligi Kuu ya England msimu huu na msimu ujao utakuwa wa kwanza kwao kutocheza Ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya tangu msimu wa 2002/03.

Pia nafasi yao pekee ya kumaliza msimu huu angalao kuweza kupata kikombe iliingia doa wiki iliyopita baada ya kutolewa na Atletico Madrid katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Europa matokeo yaliyozidi kuongeza shinikizo kwa Benitez.

Msimu wa kutetereka kwa Liverpool pia umeshuhudia kuwasili mwenyekiti mpya, huku mkuu wa Shirika la Ndege la Uingereza Broughton akiteuliwa na wamiliki wa klabu George Gillett na Tom Hicks kusimamia mauzo ya klabu.

Hata hivyo, Benitez, ambaye amekuwa akiungwa mkono hadharani na mwenyekiti mpya amesema: "Nina mkataba wa miaka minne kwa hiyo tusubiri.

"Nimekwishazungumzia uvumi huu wiki mbili au tatu zilizopita na siwezi kuendelea kuzungumzia kila wakati.