Arsene Wenger akasirikia Blackburn

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amedai mabao yote mawili ya Blackburn Rovers yasingekubaliwa kutokana na mlinda mlango wao kuzuiwa baada ya timu yake kufungwa mabao 2-1 katika uwanja wa Ewood Park.

Image caption Wenger akionesha kukasirika

Rovers walikuwa wakimjaribu mlinda mlango wa Arsenal Lukasz Fabianski kwa mipira ya juu na wakafanikiwa kufunga mabao yao yote mawili kutokana na mikwaju ya kona.

"Lengo kubwa la Blackburn ilikuwa kila mara kumzuia mlinda mlango. Sielewi kwa nini mwamuzi alikuwa anafumbia macho hali ile."

Wenger pia anahisi timu yake ilipaswa kupatiwa mkwaju wa penalti baada ya Michel Salgado kumuangusha Robin van Persie.

Meneja huyo wa Arsenal aliyewahi kulalamika namna wachezaji wake wanavyolengwa kukabiliwa kwa nguvu na timu zinazofundishwa na meneja wa Rovers Sam Allardyce, amesema hakushangazwa na namna Blackburn walivyocheza.

"Hatukuwa na bahati kwa vile tulipoteza mchezo huo, lakini hata hivyo hatukucheza vizuri pia" aliongeza meneja huyo Gunners.

Amesema"Katika soka unapokuwa hufuati mpira na unamzuia mlinda mlango asiupate mpira ni madhambi. Nadhani mwamuzi hawezi kuruhusu hali kama hiyo. Nimekatishwa tamaa kwa vile mwamuzi aliruhusu hali hiyo itokee katika mchezo wa soka na si haki kwa mlinda mlango kufanyiwa hivyo."

Naye meneja wa Rovers Allardyce amekiri timu yake ilikuwa ikimlenga Fabianski lakini akasema walikuwa wakifanya hivyo kwa kufuata kanuni.

Image caption Kocha wa Blackburn Rovers Sam Allardyce

"Tunafahamu udhaifu wa Arsenal upo ndani ya kisanduku cha hatari na tulitumia makosa yao," aliongeza Allardyce.

Timu ya Wenger imeshinda mchezo mmoja tu katika michezo minane iliyocheza katika mashindano yote na bado haina uhakika ya kudhibiti nafasi ya tatu itakayowasaidia kufuzu moja kwa moja kwa michezo ya msimu ujao ya Ubingwa wa Ulaya.

Manchester City na Tottenham, watakaopambana siku ya Jumatano, bado wanaweza kuinyakua nafasi ya Arsenal iwapo Gunners watapoteza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Fulham siku ya Jumapili.

Wenger amesema anaamini kile watakachofanya na sio Manchester City na Tottenham watafanya nini.

"Tuna mchezo wa kumalizia msimu wa ligi nyumbani na tunataka kumaliza vizuri."