Neil Lennon asubiri siku kumi

Meneja wa muda Neil Lennon ana matumaini makubwa ya kuelezwa siku chache zijazo kabla ya mchezo wa mwisho wa siku ya Jumapili wa kukamilisha msimu, iwapo amefanya ya kuridhisha ili akabidhiwe mikoba ya kudumu kuifundisha Celtic.

Image caption Scott Brown na Neil Lennon

Matokeo ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mabingwa wa Scotland Rangers ina maana Lennon ameiongoza Celtic kushinda michezo yake saba ya ligi mfululizo.

Lennon amekaririwa akisema "Nimeelezwa, tangu nilipokabidhiwa hatamu za kuifundisha timu hii, hawatanieleza chochote hadi mchezo wa mwisho ambao ni siku ya Jumapili dhidi ya Hearts."

"Kwa hiyo nitafahamu hatma yangu huenda wiki ijayo au ndani ya siku 10."

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 38 alikabidhiwa mikoba ya kuifundisha kwa muda Celtic baada ya meneja wa awali Tony Mowbray kutimuliwa kutokana na kufungwa mabao 4-0 na timu iliyo katika hatari ya kushuka daraja ya St Mirren mwezi wa Machi.

Nafasi ya meneja huyo wa zamani wa timu ya akiba ya kukabidhiwa kazi ya kudumu iliingia dosari baada ya kufungwa mabao 2-0 na klabu ya daraja la kwanza ya Ross County katika nusu fainali ya Kombe la Scotland.