Manchini kuendelea kubakia Man City

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Manchester City Khaldoon Al Mubarak, Roberto Mancini ataendelea kuifundisha klabu hiyo kwa "miaka mingi."

Image caption roberto mancini

Matumaini ya City kumaliza katika nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya England yalimalizwa siku ya Jumatano baada ya kufungwa bao 1-0 na Tottenham, ambao sasa wanaweza kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.

Lakini uvumi uliokuwepo kwamba ajira ya Mancini ilikuwa hatarini umekanushwa na Mwenyekiti wa City.

Mubarak ameeleza katika mtandao rasmi wa Manchester City "."

"Roberto ni meneja wetu. Amefanya kazi murua alipojiunga nasi katikati ya msimu na amefanikiwa kuwaweka pamoja wachezaji. Ninafuraha sana na mmiliki wa klabu Sheikh Mansour anafarijika namna alivyofanikiwa kuifikisha timu hapa ilipofika."

Mubarak ameongeza: "Tunaamini ni meneja sahihi kwa klabu yetu kwa miaka mingi. Tunachotaka msimu huu kuwa na muda wa kujiandaa na kujipanga vilivyo.

"Tunafahamu maeneo ambayo tunahitajika kujirekebisha ndani ya klabu."

Nafasi ya tano si mahali ambapo tulipataka, lakini hata hivyo ni mafanikio makubwa kutoka nafasi ya 10 hadi ya tano.

Mancini mwenyewe amekiri kuvunjika moyo kutokana na kipigo walichopata kutoka kwa Tottenham.

Kulikuwa na uvumi uliozagaa kwamba Mancini na mshambuliaji nyota Carlos Tevez hawaelewani, lakini Mubarak amesisitiza Muargentina huyo pia ataendelea kubakia katika klabu hiyo na huenda akawapiku wachezaji nyota duniani kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.