Hodgson kubakia Fulham

Roy Hodgson amesisitiza bado ataendelea kuifundisha Fulham licha ya timu hiyo kufungwa na Atletico Madrid katika fainali ya Kombe la Europa.

Image caption Hodgson kuendelea kufundisha Fulham

Hali ilionekana huenda ubingwa ungeamuliwa kwa mikwaju ya penalti hadi Diego Forlan alipofunga bao la pili katika dakika ya nyongeza ya 116 na kuiwezesha klabu hiyo ya Hispania kunyakua kombe kwa ushindi wa mabao 2-1.

Na meneja Hodgson, anayehushishwa kujiunga na vilabu mbalimbali amepongeza mafanikio ya Fulham msimu huu kwa kusema: "Ilikuwa uchungu mkubwa kufungwa".

Ameongeza:"Lakini kutokana na muda wangu ukizidi kuyoyoma, sijafikiria kuondoka. Kila mara nimekuwa mtiifu kwa Fulham na bado nitaendelea."

Hodgson amefanya mageuzi makubwa katika miaka yake miwili ya umeneja wa Cottagers, akiinusuru klabu hiyo kushuka daraja msimu wake wa kwanza, akaiongoza hadi kumaliza nafasi ya nane msimu uliopita na kwa mara ya kwanza kuipeleka hatua ya fainali ya michuano ya Ulaya msimu huu.

Katika kuthamini mafanikio yake, alitangazwa meneja bora miongoni mwa mameneja wa Ligi Kuu ya England mwaka huu.

Na kutokana na mafanikio hayo kumekuwa na uvumi unaomhusisha Hodgson mwenye umri wa miaka 62 aliyewahi kuzifundisha Inter Milan, Blackburn na timu ya taifa ya Finland huenda akajiunga na Liverpool kuchukua nafasi ya Rafael Benitez na wapo waliosema huenda akawa meneja wa England kuchukua nafasi ya Fabio Capello atakapomaliza mkataba wake kuifundisha England.

Lakini akizungumza baada ya kupoteza mchezo mjini Hamburg siku ya Jumatano, alisema: "Kamwe haijagonga mawazo yangu. Bado nina mkataba na Fulham na kwa kadri ninavyoelewa hapa ndipo nitakapokuwa msimu ujao."