Togo ruksa kushiriki michuano ya CAF

Emmanuel Adebayor aliyekuwa nahodha wa Togo.
Image caption Emmanuel Adebayor alitangaza kujitoa kuchezea timu ya taifa ya Togo kutokana na shambulio hilo.

Shirikisho la Soka Afrika, limeiondolea Togo marufuku iliyozuia taifa hilo la Afrika Magharibi kushiriki mashindano mawili ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Utekelezaji unaanza mara moja na Togo sasa itashiriki katika mashindano ya 2012.

Uamuzi wa kuiondolea Togo marufuku hiyo umetangazwa rasmi na shirikisho la soka barani Afrika, CAF, katika kikao cha maafisa wake wakuu mjini Cairo, Misri.

Caf iliiwekea Togo marufuku baada ya timu hiyo ya Hawks, yaani mwewe, ilipoamua kujiondoa katika mashindano ya mwaka 2010, ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola, baada ya basi la wachezaj wao kushambuliwa kwa risasi na baadhi ya raia wa Togo kuuawa.

CAF iligadhabishwa na hatua ya timu hiyo kujiondoa kupitia amri ya serikali mjini Lome, badala ya timu yenyewe kufanya uamuzi.

Timu ya Togo kisha ilikatazwa kushiriki katika michuano miwili, ya mwaka 2012 na 2014.

Lakini Togo ilikata rufaa kupitia mahakama ya dunia inayosikiliza kesi za michezo, na baadaye rais wa FIFA Sepp Blatter akihusika kama mpatanishi katika kuutatua mzozo huo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii