Chelsea yashinda kombe la FA

Carlo Ancelotti ameweka rekodi wakati Didier Drogba alipopachika bao kipindi cha pili na kuizamisha Portsmouth hali iliyoifanya Chelsea kuweka kibindoni makombe mawili, ubingwa wa Ligi ya England na Kombe la FA.

Image caption Droba aipa ushindi Chelsea dhidi ya Portsmouth

Shuti la Drogba la adhabu ya moja kwa moja alilopiga kiufundi ndio liliamua ushindi kwa Chelsea katika mchezo ambao Chelsea walikosa mabao mengi kipindi cha kwanza ambapo mpira ulikuwa ukigonga nguzo ya goli mara kwa mara ambapo pia timu zote zikikosa kufunga mikwaju ya penalti.

Chelsea ambayo inakuwa klabu ya saba kushinda makombe mawili katika msimu mmoja, kwa mara nyingine ilikuwa na kila jambo la kumshukuru mshambuliaji wao hatari Drogba, ambaye amezidi kuweka rekodi ya kufunga katika michezo sita iliyopia kwenye uwanja wa Wembely huku msimu huu akiwa amefunga mabao 37.

Alifunga dakika chache tu baada ya Portsmouth kukosa mkwaju wa penalti ambapo Kevin-Prince Boateng alipiga mkwaju usio wa kiufundi na kuokolewa na mlinda mlango wa Chelsea Petr Cech na ule wakati ambapo Pompey ilionekana kurejea kile ilichofanya miaka miwili iliyopita ukipotea.

Chelsea nayo ilikosa kufunga bao la pili kwa kwaju wa penalti baada ya Frank Lampard kuangushwa na Michael Brown na mkwaju wake kwenda nje.