Usain Bolt ashinda mita 100

Bingwa dunia na Olympiki wa mbio fupi Usain Bolt amekimbia kwa muda mzuri zaidi mwaka huu duniani wakati aliposhinda mbio zake za kwanza kwa mwaka 2010.

Image caption Bolt aweka muda mzuri Korea

Mkimbiaji huyo wa Jamaica alitimka kwa muda wa sekunde 9.86 katika mbio za mita 100 za Ubingwa wa Daegu huko Korea Kusini.

Bolt alianza mbio hizo kwa kujikwaa katika vibao vya kuanzia kasi lakini akaweza kuongoza katikati ya mbio hizo kabla ya kumaliza kwa ushindi.

Usain Bolt mwenye umri wa miaka 23 atakimbia tena siku ya Jumapili mjini Shangai katika mbio za mita 200 za Ligi ya Diamond.

Mjamaica mwenzake Asafa Powell naye alikimbia kwa kasi ya sekunde 9.81 na kuweza kushinda mbio za mita 100 za ufunguzi wa Ligi ya Diamond zilizofanyika Qatar siku ya Ijumaa, lakini muda huo ulionekana alisaidiwa na upepo.

Bolt alishinda medali tatu za dhahabu wakati wa mashindano ya Olympiki ya Beijing mwaka 2008 katika mbio za mita 100, 200 na mita 4x100 kupokezana kijiti na akarudia hivyo hivyo katika mashindano ya riadha ya dunia yaliyofanyika Berlin mwaka 2009 .

Katika mbio hizo za Korea Kusini, Mjamaica mwenzake ambaye walipata medali ya dhahabu pamoja kupokezana kijiti mwaka 2008 Michael Frater alishika nafasi ya pili, huku Mmarekani Mike Rodgers akishika nafasi ya tatu.

Travis Padgett, ambaye rekodi yake bora ni sekunde 9.89 alitarajiwa kutoa mkubwa upinzani kwa Bolt, lakini Mmarekani huyo alimaliza akiwa nafasi ya tano nyuma ya Bolt kwa sekunde 0.44.

Katika mbio za wanawake mkimbiaji wa Marekani wa mita 100 Carmelita Jeter alishinda baada ya kukimbia muda wa sekunde 11.00 mbele ya akina dada wawili wa Jamaica, Veronica Campbell-Brown na Sherone Simpson.