Bayern na Inter leo ni leo katika fainali

Louis van Gaal na Jose Mourinho
Image caption Patashika ya fainali kuwania taji la ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya. Makocha Louis van Gaal na Jose Mourinho wanania heshma ya kipekee.

Kocha wa Inter Milan, Jose Mourinho, amesema kitu pekee anachofikiria na kuelekeza nguvu zake ni kupata ushindi katika fainali ya Ligi ya Vilabu bingwa barani Ulaya kuliko uvumi unaozagaa kwamba yuko mbioni kuhamia Real Madrid.

Inter inakabiliana na Bayern Munich katika mechi inayochezwa Jumamosi jioni huko Madrid, Hispania.

Kocha huyo wa Inter alisisitiza: "Yoyote anayecheza fainali ya ligi ya vilabu bingwa Ulaya hawezi kufikiria jambo jingine.

"Nilitwaa taji na Porto nilijua kabla kuwa nitahamia Chelsea, lakini kwa sasa siwezi kujua... siifahamu Real Madrid."

Mourinho mwenye umri wa miaka 47 aliongeza angepumzika "siku nne au tano" baada ya fainali kuamua mwelekeo anaotaka kufuata.

Rekodi mpya

Mourinho aliwahi kufanya kazi chini ya kocha wa Bayern, Louis van Gaal katika timu ya Barcelona na makocha wote wanawania heshma ya kuungana na Ernst Happel na Ottmar Hitzfeld, kushinda ligi ya vilabu bingwa wakiwa na timu mbili tofauti.

Baada ya kuendeleza mafanikio aliyoyapata Porto kwa kuchukua vikombe vya ligi akiwa na Chelsea na sasa Inter, kocha huyo wa kireno anawaniwa kwa nguvu na timu kubwa duniani huku Real Madrid wakiongoza harakati hizo, lakini anadai kinachomvutia kwasasa ni fainali hiyo tu.