Blackpool 3 Cardiff 2

Ikiwa nyuma mara mbili Blackpool iliweza kujitutumua na kufanikiwa kuilaza Cardiff na kufanikiwa kupanda daraja masimu ujao. Sasa itacheza Ligi Kuu ya Soka ya England maarufu Premier League. Katika mpambano uliofanyika uwanja wa Wembley huku kukiwa na jua kali.

Image caption Ormerod akishangilia bao la tatu la Blackpool

Blackpoo ama maarufu kwa jina la The Tangerines walishinda pambano hilo kwa mabao 3-2, ambapo mabao yote yakiwa yamefungwa kiufundi kipindi cha kwanza na kwa baadhi ya nyakati ni kutokana na makosa ya walinzi.

Wachezaji wa timu zote mara kwa mara iliwabidi wajipooze kwa kunywa maji kutokana na jua kali.

Michael Chopra na Joe Ledley mara mbili waliifungia mabao Cardiff na kuwafanya waongoze, lakini shuti la adhabu ndogo la moja kwa moja lililofumuliwa kiufundi na Charlie Adam pamoja na bao la karibu na lango la Gary Taylor-Fletcher yaliiwezesha klabu hiyo ya Lancashire kusawazisha kabla Brett Ormerod kupachika bao la tatu la ushindi kabla ya mapumziko.

Matokeo hayo yanakamilisha msimu uliokuwa na jitahada kubwa ya wachezaji wa Blackpool, ambao sasa watacheza mashindano makubwa tangu mwaka 1971.

Pia ni mafanikio makubwa kwa meneja Ian Holloway, ambaye mikakati yake ya ushambuliaji kwa mwaka mzima na pia katika uwanja wa Wembley imeisaidia timu yake kushinda kwa mfumo wa uchezaji wa 4-3-3.

Blackpool inaweza kuonekana ni klabu ndogo kuweza kucheza Ligi Kuu ya England, lakini hivi sasa wanajinoa kukabiliana bega kwa bega na wachezaji mahiri wa Engaland baada ya kushinda mchezo ambao umewapatia kitita cha paundi za Uingereza milioni 90.