Mnigeria Dangote akanusha hisa Arsenal

Mfanyabiashara raia wa Nigeria Aliko Dangote amekanusha kwamba ana mipango ya kununua asilimia 15 ya hisa za klabu ya Ligi Kuu ya England ya Arsenal.

Image caption Aliko Dangote tajiri wa Nigeria

Awali kulikuwa na uvumi anakusudia kujiingiza katika mchakato wa hisa za Lady Nina Bracewell-Smith zenye thamani ya paundi milioni 100.

Katika taarifa yake, Dangote amethibitisha, "alihusishwa katika mazungumzo juu ya kuwekeza siku zilizopita".

Lakini akaongeza: "Kimsingi ninachoweza kusema kwa wakati huu sina nia ya kuwekeza katika klabu hiyo na sitaomba hisa."

Dangote, ambaye ni Rais na mtendaji mkuu wa kampuni ya Dangote Group, anaheshimika kuwa Mwafrika tajiri zaidi, huku gazeti la Forbes nchini Marekani likikadiria miaka miwili iliyopita alikuwa na utajiri wa dola bilioni 3.3 sawa na paundi bilioni 2.3.

Utajiri wake unatokana na himaya kubwa ya biashara aliyojijengea tangu mwaka 1977 na sasa anamiliki kampuni kubwa ya sukari nchini Nigeria, kiwanda cha saruji na cha nguo.

Hivi karibuni aliliambia gazeti moja la Nigeria amekuwa mpenzi wa Arsenal kwa muda mrefu na akaongeza: "Ilikuwa mwaka 1980 wakati nilipofanya urafiki na Bw David Dein, makamu mwenyekiti wa zamani wa bodi ya Arsenal."

Mwezi uliopita, Lady Bracewell-Smith aliiagiza kampuni ya udalali ya Uingereza ya Blackstone kutafuta mnunuzi wa hisa zake, ambapo mwaka 2008 alijiondoa katika bodi ya Arsenal.

Stan Kroenke na Alisher Usmanov ni wanahisa wawili wakubwa Arsenal na ilikuwa ikihofiwa uamuzi wa Lady Bracewell wa kuuza hisa zake huenda ungezua uhasama baina yao.