Muimbaji ufunguzi Kombe la Dunia afariki

Muimbaji wa mtindo wa opera aliyeteuliwa na Nelson Mandela kuimba wakati wa sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia amefariki dunia baada ya kuuguwa homa ya uti wa mgongo.

Siphiwo Ntshebe, mwenye umri wa miaka 34, alilazwa hospitali mjini Port Elizabeth wiki iliyopita na alifariki dunia siku ya Jumaanne kwa mujibu wa kampuni inayouza nyimbo zake, Epic Records.

Alitazamiwa kuimba wimbo wake mpya "hope" katika sherehe za ufunguzi tarehe 11 mwezi wa Juni mjini Johannesburg. Wimbo huo una ujumbe maalum wa matumaini na imani uliotungwa na kutolewa na Bwana Mandela.

Mwaandishi wa BBC mjini Johannesburg, Pumza Fihlani anasema Ntshebe hakuwa maarufu sana nchini Afrika Kusini. Hata hivyo kwa yeye kutumbuiza katika sherehe za Kombe la Dunia kungempa fursa ya kujulikana zaidi nchini mwake