Tanzania yanyukwa 5 - 1 na Brazil

Image caption Kaka alifunga mojawapo ya magoli ya Brazil.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taif Stars, ikicheza mbele ya maelfu ya mashabiki wake, ilichapwa magoli 5-1 katika mechi ya kujipima nguvu iliyofanyika Jumatatu jioni katika uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.

Mshambuliaji Robinho ndiyo aliwapatia Brazil goli la kwanza, kabla ya kuongeza la pili kwenye mechi ambayo si makosa kusema Taifa Stars walicheza vizuri ingawa tatizo la kawaida limekuwa likijirudia - kukosekana kwa maarifa ya kufunga.

Shambulio la Kaka na mengine mawili kutoka kwa mchezaji wa akiba, Ramires yalikamilisha magoli kwa The Selecao, lakini Stars walionekana kuwachokoza Brazil ambapo katika dakika ya sita Mrisho Ngassa alikosa goli la wazi.

Taifa Stars walipata goli la kufutia machozi kupitia Jabir Aziz, mchezaji wa akiba aliyemalizia kwa kichwa mpira wa kona.

Kocha wa Brazil, Dunga alisisitiza kuwa mechi hiyo haikuwa ya ushindani, bali ilitumika kuandaa kikosi chake kwa Kombe la Dunia.

Mchezaji muhimu aliyekosekana ni mlinda mlango namba moja Julio Cesar aliyejeruhiwa katika mechi ya majaribio dhidi ya Zimbabwe juma lililotangulia, badala yake alicheza mlangoni alicheza Heurelho Gomes.