Gari la mafuta laangamiza 220 Kongo

Zaidi ya watu 220 wanahofiwa kufa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Watu hao wameangamia baada ya lori moja lilobeba mafuta kuanguka na kuwaka moto katika kijiji cha Sange, mashariki mwa nchi hiyo.

Inaarifiwa kuwa watu hao walikuwa wakijaribu kuchota mafuta kutoka lori hilo, lilokuwa limepinduka, baada ya dereva wake kushindwa kulidhibiti.

Baadhi ya waliokufa walikuwa wakichota mafuta yaliyokuwa yakivuja, lakini walinaswa ndani ya majengo, ikiwa ni pamoja na ukumbi wa sinema.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliungana katika jitihada za kuokoa waliojeruhiwa.

Walioshuhudia wanasema moto uliangamiza idadi kubwa ya nyumba.

Janga

"Watu walijaribu kukimbia, lakini walinaswa na moto huo mkali uliowaangamiza na kuwa majivu," Tondo Sahizira, 28, alilieleza shirika la habari la AFP.

Ajali hiyo ilitokea Ijumaa jioni eneo la Sange, yapata kilometa 70 kusini mwa mji wa Bukavu, Kivu Kusini.

Gari hilo lililokuwa likisafiri kutoka Tanzania, lilipinduka na mafuta kuanza kuvuja.

"Mafuta yalianza kuvuja, lakini badala ya watu kukimbia, walianza kuchota mafutal," alisema Bw Sahizira.

"Dakika chache baadaye kulikuwa na mlipuko, miale ya moto ilifumuka na kusambaa kwa kasi."

Nyumba kadhaa zilizoezekwa nyasi ziliwaka moto, vile vile ukumbi uliokuwa ukitumika kuonyesha mechi za Kombe la Dunia.

Madnodje Mounoubai, msemaji wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa, alisema idadi ya vifo huenda ikaongezeka.