Steven Gerrard ajifunga kusalia Liverpool

Image caption Steven Gerrard kipenzi cha mashabiki wa Liverpool, sasa amesema atasalia kuichezea timu hiyo.

Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, ameihakikishia timu yake kuwa ataendelea kubakia Anfield, msimu ujao.

Licha ya kusaini mkataba mpya unaompa nafasi ya kuchezea Liverpool mpaka Juni 2013, taarifa zilieleza kuwa Gerrard angeomba uhamisho msimu huu.

Lakini baada ya kukutana na meneja Roy Hodgson, sasa ameweka wazi kuwa yuko tayari kuendelea kucheza Liverpool.

"Nilitaka fursa ya kukutana faragha na Roy Hodgson," mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 aliieleza tovuti ya Liverpool. "Nimefurahishwa na mipango aliyonayo kwa timu."

Aliongeza: "Ndiyo kwanza nilirejea mazoezini siku ya Jumatatu huko Melwood pamoja wachezaji wengine waliocheza Kombe la Dunia lakini nina shauku sana na msimu mpya."

Kulikuwa na tetesi kuwa Gerrard angeweza kujiunga na meneja Jose Mourinho katika klabu ya Real Madrid, tangu alipoongoza timu ya England na kupata matokeo mabaya kwenye Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.