Liverpool haitamwuza Mascherano bei poa

Image caption Javier Mascherano anataka kuhama England baada ya mkewe kukataa kuishi nchi hiyo.

Meneja wa Liverpool, Roy Hodgson, amesisitiza kuwa hatamwuza kwa bei ya kutupa kiungo wake Javier Mascherano, ambaye amekuwa akitaka kuhama timu hiyo yenye ngome yake Anfield.

Nahodha huyo wa Argentina, mwenye umri wa miaka 26, ana miaka miwili imesalia kwenye mkataba wake, lakini anataka kuhama kutokana na sababu za kifamilia huku kukiwa na taarifa kuwa Inter Milan wanaweza kumchukua.

Lakini Hodgson alisema: "Tunataka dau linalolingana na kile tunachodhani ndiyo thamani yake halisi.

"Kama klabu inayomtaka itashindwa kufikia dau hilo, basi atabakia. Au tunapata mnunuzi anayefikia, hapo anaweza kwenda."

Baada ya kurejea kutoka Kombe la Dunia mwezi Julai, Mascherano alieleza kuwa alitaka kuhama kutoka Anfield, ingawa Hodgson anataka kiungo huyo aendelee kubakia katika timu yake.

Hodgson bado hajapokea ombi la kumnunua Mascherano, na aliongeza kuwa mchezaji huyo wa Argentina, ambaye mkewe amekataa kuhamia England, anaelewa hali ya klabu yake.