Kim Clijsters bingwa Marekani

Kim Clijsters na Vera Zvonareva
Image caption Kim Clijsters ni mshindi wa mashindano matatu makubwa ya Grand Slam ya New York

Bingwa mtetezi wa mashindano ya Marekani ya tennsi ya US Open, Kim Clijsters kutoka Ubelgiji, alifanikiwa kumshinda Vera Zvonareva katika pambano la dakika 59, na kwa mara ya tatu kuwa bingwa wa mashindano hayo yaliyofanyika Flushing Meadows mjini New York.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, baada ya kustaafu na kupumzika kwa muda, mwaka jana alirudi katika mashindano ya tennis na kuweza kupata ushindi.

Jana aliweza kumshinda mpinzani wake kutoka Urusi kwa 6-2 6-1.

Katika fainali hiyo ya Jumamosi, tarehe 11 Septemba, ilikuwa wazi kwamba Zvonareva alikuwa amelemewa.

Ubingwa wa Clijsters katika mashindano makubwa ya Grand Slam, umepatikana katika mashindano ya New York.

Clijsters alipata ushindi wake wa kwanza wa Grand Slam mwaka 2005.

Kwa upande wa fainali za wanaume Jumapili usiku, Rafael Nadal wa Uhispania atajaribu kuwa mtu wa saba duniani kuwahi kushinda mashindano yote manne makubwa ya Grand Slam, wakati atakapopambana na Novak Djokovic kutoka Serbia.

Djokovic alifanikiwa kuingia fainali baada ya kumshinda Roger Federer katika nusu fainali, 5-7 6-1 5-7 6-2 7-5, na kukomesha rekodi yake ya kufika fainali za mashindano ya Flushing Meadows, kwani amekuwa akifuzu kuingia fainali, miaka sita mfululizo.