Nadal athibitisha ni nambari 1

Mhispania Rafael Nadal alifanikiwa kuingia fainali ya mashindano ya tennis ya ATP mjini London, kwa kumshinda Muingereza Andy Murray katika nusu fainali ya kusisimua iliyochezwa Jumamosi.

Image caption Nadal anatazamiwa kuwa bingwa wa mashindano ya kumalizia msimu ya ATP

Licha ya Andy Murray kumtikisa na kumbabaisha mchezaji nambari moja duniani, Nadal hatimaye aliweza kujikakamua na kupata ushindi wa 7-6 (7-5) 3-6 7-6 (8-6).

Nadal, mwenye umri wa miaka 24, sasa atapambana katika fainali ya Jumapili, tarehe 5 Novemba.

Inaelekea itakuwa vigumu kumzuia Nadal kuchukua ubingwa katika mashindano haya ya kumalizia msimu, kwani tayari ameweka kibindoni ubingwa wa mashindano matatu, kati ya manne, ya mashindano makubwa ya Grand Slam msimu huu.

Iwapo atanyakua ushindi Jumapili, basi huu utakuwa ni ubingwa wake wa kwanza katika mashindano ya ATP ya kumalizia msimu.

"Leo nimeweza kucheza vizuri zaidi katika maisha yangu ya tennis", alielezea Nadal baada ya ushindi wa Jumamosi.

"Ni mchana uliokuwa na hisia nyingi kwangu. Unafahamu mambo yalivyokuwa magumu kwangu mwaka uliopita. Kuwa katika fainali ni ndoto iliyotimia".