Li Na ni bingwa wa kina dada French Open

Li Na Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mchezaji wa kwanza kutoka bara Asia kupata ubingwa wa Grand Slam mapambano ya mchezaji mmoja kwa mmoja

Li Na kutoka Uchina, ameandikisha historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka bara Asia kufanikiwa kutwaa ubingwa katika mashindano makubwa ya kiwango cha Grand Slam, baada ya kumshinda bingwa mtetezi Francesca Schiavone kutoka Italia katika fainali ya French Open siku ya Jumamosi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, anashikilia nafasi ya saba katika orodha ya wachezaji bora wa kike ulimwenguni, alishindwa katika fainali ya Australian Open mapema mwezi Januari mwaka huu.

Alimshinda Schiavone 6-4 7-6 (7-0).

Tangu mwanzo Li alionyesha umahiri wake, na licha ya kuingiwa na wasiwasi baadaye katika pambano hilo, aliweza kumvua Schiavone ubingwa baada ya saa nzima, na dakika 48.

Kabla ya pambano la Jumamosi, wachezaji hao waliwahi kutoana jasho mara nne katika mapambano ya awali, ikiwa ni pamoja na Schiavone kutwaa ushindi katika pambano lao la Roland Garros, Ufaransa, mwaka uliopita.

Li hapendi sana kucheza katika uwanja wa udongo, kinyume na mpinzani wake katika fainali, ambaye ana umaarufu wa kuwika katika viwanja vya aina hiyo.