Rafael Nadal ni bingwa wa French Open

Mchezaji bora zaidi wa kiume duniani hivi sasa, Rafael Nadal, aliweza kuonyesha uzoefu wake katika uwanja wa udongo mjini Paris, kwa kuwa mshindi wa French Open kwa mara ya sita.

Nadal, mwenye umri wa miaka 25, aliweza kuifikia rekodi ya Bjorn Borg kutoka Sweden, ya kupata ushindi mara sita katika uwanja huo wa Roland Garros, alipomshinda Federer, kutoka Uswisi,

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Amepata ubingwa wa French Open mara sita

7-5 7-6 (7-3) 5-7 6-1 katika pambano la kusisimua ambalo lilifanyika kwa muda wa saa tatu na dakika 39.

Nadal, ambaye kwa jumla sasa amekuwa mshindi wa mashindano makubwa ya Grand Slam mara kumi, alijihakikishia pia kuendelea kuongoza orodha ya wachezaji bora duniani, kwa kumtangulia Novak Djokovic kutoka Serbia.

Katika pambano la kusisimua, mchezaji huyo kutoka eneo la Majorca nchini Uhispania, ilimbidi kupambana vikali baada ya wakati fulani kushindwa kutumia nafasi nzuri ya kupata ushindi alipokuwa anaongoza kwa seti mbili.

Federer, mwenye umri wa miaka 29, alikuwa ameanza kwa kasi kama ile iliyomwezesha kumshinda Djokovic katika nusu fainali, ambapo kabla ya hapo, alikuwa hajashindwa katika mapambano 43.

Nadal alionekana kuwa na wasiwasi wakati seti ya kwanza ilielekea kumwendea Federer, hasa matokeo yalipokuwa 5-3.

Hata hivyo baadaye aliweza kuwa na imani ya kufanya vyema, na ghafula Nadal alianza kucheza kwa jitihada, na kuutandika mpira kwa kasi ambayo kwa kawaida imemsaidia kupata ushindi katika mashindano mengi, na kuendelea kuvuma katika uwanja wa Roland Garros.