Cameroon yatoka sare 0-0 na Urusi

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Stephane Mbia wa Cameroon

Cameroon ilitoka sare tasa na Urusi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa japo timu zote mbili zililaumiwa kuweka wachezaji dhaifu katika mji wa Salzburg nchini Austria .

Urusi walitawala mechi hiyo lakini ni Cameroon iliyonusia zaidi kufunga bao.

Licha ya kipa Vyacheslav Malafeev wa Urusi kulemewa, bado mlinzi wa Cameroun Aurelien Chedjou's aliambulia patupu na mpira kupiga chuma.

Kocha wa Urusi Dick Advocaat alikosea kwa kumpumzisha mshambulizi wa Tottenham Roman Pavlyuchenko, aliyesaidia kuifunga Armenia katika mechi yao ya Jumamosi na kwa upande wa Cameroon walimtamani Alex Song ambaye hangecheza kutokana na jeraha.

Timu ya Indomitable Lions imeshindwa kufunga hata bao moja katika mechi zake tatu ilizocheza hivi punde licha ya kujivunia kuwa na mshmbuliaji wa kati bora zaidi duniani, Samuel Eto'o.

Mechi hiyo iliyotoka sare tasa inafuata nyingine waliocheza na Senegal na kutoa matokeo kama hayo siku ya Jumamosi.

Na waliposhindwa kuifunga Teranga Lions katika mechi muhimu ya kufuzu kwa kombe la taifa bingwa barani Afrika mwaka wa 2012, kulitokea rabsha kutokana na ghadhabu za mashabiki mjini Yaounde.

Sasa wakiwa na pointi tano nyuma ya Senegal inayoongoza kundi lao la E, washindi hao mara nne wa Afrika wanatishiwa kukosa kufuzu kwa fainali za mwaka ujao nchini Equatorial Guinea na Gabon.