Ghana mboga kwa Korea Kusini

gyan
Image caption Asamoah Gyan aliipatia Ghana bao lao la pekee

Koo Ja-Cheol aliipatia Korea Kusini bao la ushindi lililoiwezesha Korea Kusini kushinda Ghana kwa mabao 2-1 kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa iliofanyika katika uwanja wa Jeonju World Cup.

Korea ilifunga mwanzo kupitia Ji Dong-won kunako dakika ya 12 alipopiga mpira kwa kichwa huku kipa wa Black Stars Richard Kingston akidaka hewa. Mshambuliaji maarufu wa Ghana Asamoah Gyan ambaye alitia fora kombe la dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini nusra aipatie timu yake bao la kusawazisha lakini hakuwa na bahati.

Bao la kusawazisha

Black Stars ilipata bao la kusawazisha dakika ya 65 wakati Sulley Muntari alipovinjari na kumpa Gyan pasi murwa ya chini aliyotuliza kimyani.

Furaha ya Black Stars kusawazisha ilikatizwa sekunde chache baadae Koo alipofunga bao la ushindi la Korea.

Hii ni mara ya kwanza kwa kocha wa Black Stars Goran Stevanovic kupoteza mechi tangu achukue usukani kama kocha wa Ghana, ikiwa ni mechi yake ya tano.