Uefa haitokubali vilabu vyenye madeni

Shirikisho la soka barani Ulaya -Uefa limeanzisha sheria katika kujaribu kuhakiki kuwa vilabu vinatumia fedha kadri ya uwezo wao.

Vilabu 72 ambavyo vinazidi kukabiliwa na kiwango kikubwa cha madeni vilikuwabaliana kimsingi juu ya sheria hio kwenye mkutano wao wa kila mwaka.

Mwenyekiti wa muungano wa vilabu vya soka, Greg Clarke alisema baada ya kikao kuwa ni hatua muhimu katika soka ya kulipwa.

Ameongezea kuwa sheria hiyo itasaidia vilabu viweze kudhibiti mapato yake.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mishahara itachunguzwa

Muungano huo vilevile uliunga mkono hatua hizo mpya kwenye mkutano wa Uefa nchini Cyprus kufuatia hotuba ya mkuu wa Uefa wa kitengo kinachohusiana na usawa wa matumizi ya fedha, Andrea Traverso.

Mkuu wa muungano wa vilabu, Clarke aliiambia BBC michezo kuwa Vilabu vilivyoko katika Ligi ya soka vina jumla ya madeni yanayokadiriwa kuwa pauni za Uingereza milioni 700.

Haki miliki ya picha AP
Image caption David Bernstein

Mwenyekiti wa chama cha mpira cha England David Bernstein amelielezea tangazo hilo kama la kuvutia mno.

Itakumbukwa kuwa Katibu Mkuu wa FA Alex Horne alifahamisha Kamati maalum ya Bunge mapema mwaka huu kuwa angependelea hatua kama hizo zianzishwe.

Chini ya sheria hiyo vilabu viwili vya Ligi ya England, Chelsea na Manchester City, vilivyo kileleni mwa Ligi kuu ya England vinaweza kujikuta matatani.

Hata hivyo vilabu hivyo vina mda wa msimu mzima kabla ya sheria hiyo kutekelezwa ambapo Uefa itakuwa na uwezo wa kusimamisha klabu yoyote itakayokiuka sheria hiyo.

Utafiti uliofanywa na idara ya michezo ya BBC imegundua kuwa kwa hali ilivyo Chelsea na Manchester City vingehesabiwa kuwa vilivyovunja sheria.

Man City ilitumia pauni milioni £110 zaidi ya mapato yao huku Chelsea ikionekana kuwa na deni la zaidi ya pauni milioni £50m.

Kwa kifupi sheria hiyo hairuhusu vilabu kutumia fedha zaidi ya mapato yao kibiashara.