Daniela Hantuchova baada ya kujaribu kumshinda Venus Williams mara 11 hatimaye amshinda katika mashindano ya kimataifa ya tennis ya Aegon na kufuzu kwa nusu fainali

Daniela Hantuchova alifanya kazi ya ziada na baada ya kujaribu mara 11, hatimaye aliweza kumshinda Mmarekani Venus Williams katika robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Aegon, Eastbourne nchini Uingereza, na kufuzu kwa pambano la nusu fainali ya mashindano hayo ya tennis.

Hatuchova, kutoka Slovakia, ambaye alishikilia nafasi ya pili katika mashindano ya wiki iliyopita ya Aegon Classic mjini Birmingham, alianza vyema mashindano ya Alhamisi.

Image caption Alifanya kazi ya ziada na kumshinda Mmarekani Venus Willliams

Mmarekani Williams alianza kuonyesha uhodari siku zake za kuwika katika tennis, huku upepo ukianza kuvuma mno.

Lakini Hantuchova alijitahidi na kujibu mashambulio yote, kiasi cha kuibuka mshindi kwa 6-2 5-7 6-2.

"Nahisi nilijitahidi na kucheza vyema mapema katika pambano hilo", alielezea mchezaji huyo anayeshikilia nafasi ya 29 katika orodha ya wachezaji bora duniani.

"Lakini upepo ulijitokeza kuyafanya mambo kuwa magumu kwa sisi wote wawili. Ikawa ni mchezo wa kiakili, na nilifuzu".

"Huu ndio wakati bora zaidi kwangu, msimu ya kuchezea katika nyasi, na ninahisi niko katika hali nzuri".

Hantuchova ilibidi afanye kazi ya ziada, hasa baada ya kushindwa kutumia hali ya kuongoza, akiwa na 4-2 katika mchezo, katika seti ya pili, na kumruhusu Williams kusawazisha, na kisha kulemewa 2-1 katika seti ya tatu, na kabla tu ya kupata ushindi.