Kocha wa Porto Andre Villas-Boas anajiandaa kujiunga na Chelsea kufuatia Carlo Ancelotti kufutwa kazi mwezi Mei

Inaelekea meneja wa Porto ya Ureno, Andre Villas-Boas, anajitayarisha kujiunga na klabu ya Chelsea, kufuatia Carlo Ancelotti kufutwa kazi mwezi Mei.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Kuna uwezekano atakuwa meneja mpya wa Chelsea

Kocha Villas-Boas, mwenye umri wa miaka 33, msimu uliopita aliiongoza Porto kupata ubingwa wa ligi ya Europa.

Mreno huyo, katika mkataba wake, ana kipengele ambacho kinamruhusu kuondoka Porto, iwapo klabu kitajitokeza na kuwa tayari kuzipata huduma yake kwa pauni milioni 13.2.

Katika taarifa, Porto ilielezea kwamba inatazamia kupata maelezo ambayo yatahibitisha anaweza kuondoka kwa kuzingatia kipengele hicho.

"Hadi hivi sasa klabu hakijapokea mawasiliano yoyote kuonyesha kwamba kipengele hicho kitatumika, wala makubaliano yoyote ya kocha huyo anayehitajika," taarifa ilielezea.

Inter Milan pia imehusishwa na Villa-Boas, lakini kipengele hicho katika mkataba wake wa Porto ilikuwa vigumu kukizingatia.

"Villas-Boas anatupenda, nasi tunampenda, " mkurugenzi wa michezo wa Inter Milan, Marco Branca alieleza.

"Alikuwa nasi kwa karibu muda wa miaka miwili.

"Lakini hali ni kwamba alikuwa na kipengele kilichombana kama mchezaji. Kipengele cha kuondoka kilikuwa ni cha Euro milioni 15.

Hatutaki kumpa kazi yeye na vilevile Porto!"

Klabu ya Chelsea imetangaza kwamba inanuia kutoa tangazo kumhusu meneja wao mpya katika kipindi cha siku chache zijazo.

Rais wa Porto, Pinto da Costa, amesema klabu hakiwezi kumzuia Villas-Boas kuondoka ikiwa masharti yote yametekelezwa.