Uchaguzi wa kandanda Kenya Agosti 13

MacDonald Mariga Haki miliki ya picha Google
Image caption MacDonald Mariga

Hatimaye uchaguzi wa kandanda wa kitaifa nchini Kenya utafanyika mwezi Agosti tarehe 13, ametangaza mwenyekiti wa bodi inayosimamia uchaguzi huo (IEB) Joe Okwach.

Akihutubia waandishi wa habari Alhamisi wiki hii mjini Nairobi Okwach alisema shirikisho linalosimamia mchezo huo duniani Fifa ama serikali ya Kenya ndio watakaogharamia uchaguzi huo ambao utahusisha zaidi ya vilabu elfu mbili.

Uchaguzi huo utagharimu kama dola 500,000.

Uchaguzi

Okwach ameeleza hawangeweza kuandaa uchaguzi mwezi Aprili kama walivyotangaza Disemba mwaka jana kwa sababu ya mambo mengi waliohitajika kufanya kabla ya siku hiyo.

Uchaguzi huu unatarajiwa kumaliza mzozo ambao umekumba usimamizi wa kandanda nchini Kenya tangu mwaka 2004. Kwa sasa kuna vyama viwili, Football Kenya Limited (FKL) ambayo inatambuliwa na Fifa na Kenya Football Federation (KFF) chini ya uongozi wa Sam Nyamweya naye Mohammed Hatimy ni kinara wa FKL. Wote hao watagombea uenyekiti.

Mbali na Nyamweya na Hatimy, wengine watakaogombania uenyekiti ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya Sammy Shollei, naibu wa mwenyekiti wa KFF Twaha Mbarak na mfanya biashara Mohammed Hussein.