Connor Wickham kujiunga na Sunderland

Image caption Connor Wickham

Wickham, mwenye umri wa miaka 18, anaweza kuwa mchezaji wa Sunderland katika muda wa saa 24, iwapo watakubaliana juu ya masuala binafsi pamoja na kukamilisha uchunguzi wa kiafya.

Kandarasi hiyo ya mchezaji wa timu ya taifa ya England ya vijana wasiozidi miaka 21, ambaye alianza kuchezea Ipswich akiwa na miaka 16, huenda ikafika kiwango cha pauni za Uingereza milioni £12.5m.

Awali ilidhaniwa angejiunga na timu ya Tottenham au Liverpool.

Haikufahamika mustakabali wake kwenye timu hiyo ungekuwaje, licha ya kuongeza kandarasi yake na Ipswich hadi mwezi Aprili 2014.

Historia fupi

Wickham alijumuishwa kwenye timu ya England ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21 kwa michuano ya bara Ulaya lakini hakucheza mechi hata moja.

Tangu kujiunga na Ipswich mwezi Julai 2008 amechezea kikosi cha kwanza mara 37 na kuingia kama mchezaji wa akiba mara 35,kwa jumla akifunga magoli 15.

Mwezi wa Mei 2010 Wickham alisaidia England kupata ushindi kwenye michuano ya bara Ulaya ya vijana wasiozidi miaka 17, baada ya kufunga bao la ushindi. Katika fainali hiyo England iliifunga Uhispania 2-1.

Kocha wa Ipswich Paul Jewell alisema wiki iliopita kwamba alitarajia timu nyingi kuonyesha nia ya kumsajili Wickham lakini wao hawakuwa na haraka ya kumuuza mshambulizi huyo.